Jaji Warioba: Napongeza CCM kwa hatua zake dhidi ya rushwa

0

MAKAMU wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba, amepongeza hatua zilizoanza kuchukuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mapambano dhidi ya rushwa kwenye uchaguzi.

Jaji Warioba ametoa pongezi hizo akirejea mabadiliko ya Katiba ya CCM yaliyofanywa na Mkutano Mkuu Maalum wa CCM, yakiwemo marekebisho ya namna ya kupata wagombea wa udiwani, uwakilishi na ubunge, kwa kuongeza idadi ya wapiga kura wa vikao vya kura za maoni.

Aliesema kwa kuwa vita dhidi ya rushwa si ya siku moja, CCM haina budi kuhakikisha mapambano ya kumshinda adui huyo yanakuwa endelevu kwa kusimamia misingi ya kuanzishwa kwa chama hicho.

Warioba, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Mstaafu, amesema hayo katika mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, baada ya Balozi Nchimbi kumtembelea nyumbani kwake, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kumjulia hali.

Aidha, Jaji Warioba, mbali na kukumbusha kuhusu misingi ya CCM, alisisitiza sifa na miiko ya uongozi ilivyoainishwa kwenye Katiba ya CCM, akisema chama kina wajibu wa kuendelea kuwapatia matumaini Watanzania kwa kutoa uongozi bora kwa mwelekeo sahihi wa nchi.

“Hivi mlivyoanza ni safi, in the long run (hatimaye huko mbele) tutakuwa na mwanga wa mapambano dhidi ya rushwa. Nilikuwa very interested (na hamu kubwa) kujua mabadiliko hayo kwenye Katiba ya Chama, nilivyoshindwa kuwepo kwenye Mkutano Mkuu Maalum. Ni muhimu sana CCM iendelee kusimamia misingi yake, ikiwemo ahadi za mwanachama.

“Vita hii si ya siku moja, ni muhimu muda wote chama kitafute njia za kuzuia rushwa kwa kusimamia misingi yake. Watu wazungumzie sifa na miiko ya uongozi. Wazungumzie sera, si hela. Kihistoria, CCM ni chama cha itikadi, sera na ilani. Kina wajibu wa kuonesha matumaini wapi tunawapeleka watu,” alisema Jaji Warioba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here