Idadi ya wanaopata huduma za kifedha yaongezeka Tanzania

0

Na Mwandishi Wetu

MALKIA Maxima wa Uholanzi ameipongeza Tanzania kwa ukuaji wa huduma jumuishi za fedha nchini, ambapo idadi ya watanzania wanaopata huduma za kifedha imepanda kutoka asilimia 17% kwa mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 58% kwa mwaka 2022.

Akizungumza alipokutana na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga, jijini Dar es Salaam, Malkia Maxima ambaye pia ni Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Huduma Jumuishi za Fedha, alisema kuwa pamoja na kuongezeka kwa watumiaji wa huduma za kifedha nchini, idadi kubwa ya watanzania bado wanafanya malipo kwa kutumia pesa taslimu hivyo kupunguza ukuaji wa malipo ya kidijitali.

“Malipo ya Kidijitali yatachochea ukuaji wa biashara, kuongeza uwazi na hata kuwezesha watumiaji wa huduma za kifedha kupata mikopo kwa urahisi” alisema.

Malkia Maxima aliongeza kuwa, ili kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma za kifedha hadi asilimia 100% ni muhimu kuangalia kama wateja wanamudu gharama ya huduma za kifedha, namna ya kuhusisha sekta za kiuchumi kama kilimo pamoja jinsi gani mabenki na kampuni za mawasiliano zinatumia teknolojia kuleta mabadiliko.

Awali, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga alieleza kuwa BoT inatayarisha mpango wa kuendeleza utekelezaji wa huduma jumuishi za fedha unaolenga kuongeza idadi ya wananchi wanaofikiwa na huduma za fedha nchini na kwa bei rahisi.

“Benki Kuu ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo utakaohakikisha kuwa huduma jumuishi za kifedha zinapatikana kwa urahisi au bila malipo” alisema.

Gavana Luoga aliongeza kuwa “kwa kushirikiana na timu maalum iliyoambatana na Malkia Maxima, kutakua na mpango wa tatu wa kuratibu jinsi gani ya kupanua wigo wakupeleka huduma jumuishi za kifedha kwa wananchi.

Malkia Maxima alikuja Tanzania mara ya kwanza mwaka 2010 wakati ambapo BoT inaanza mchakato wa kutekeleza huduma jumuishi za fedha. Pia alikuja 2013 na kuzindua mpango maalum wa kwanza utekelezaji wa huduma jumuishi za fedha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here