Huduma za upasuaji zazinduliwa hospitali ya Wilaya Kibaha

0

WANANCHI wa Wilaya ya Kibaha sasa wameondokana na adha ya kusafiri umbali wa Kilomita 40 kufuata huduma za upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi, baada ya Mwenge wa Uhuru kuzindua rasmi huduma hizo katika Hospitali ya Wilaya ya Kibaha.

Huduma hiyo muhimu ilizinduliwa Aprili 8 na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ussi, ambaye aliipongeza Serikali kwa hatua hiyo kubwa ya kuwasogezea wananchi huduma za afya karibu na makazi yao.

Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Christopher Ngendello, Serikali kuu ilitoa Shilingi Milioni 300 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba muhimu vya kutoa huduma za upasuaji.

“Vifaa tulivyonunua ni pamoja na mashine ya usingizi, mashine ya kemia, vitanda 30, magodoro 30, makabati ya dawa, jokofu za kuhifadhia damu, viti vya kuchangia damu pamoja na vifaa vya upasuaji,” alisema Dkt. Ngendello.

Dkt. Ngendello aliongeza kuwa huduma hiyo ilianza kutolewa tangu mwezi Machi mwaka huu na hadi kufikia Aprili 8, tayari wagonjwa 16 wamehudumiwa kwa mafanikio.

“Huduma hii imesaidia kupunguza gharama kwa halmashauri kati ya Shilingi Milioni 24 hadi 30 ambazo zilikuwa zikitumika kwa mafuta na matengenezo ya magari ya kubebea wagonjwa waliokuwa wakisafirishwa hadi Tumbi,” alieleza.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru, Ismail Ussi aliwasihi wananchi kuitunza miundombinu ya hospitali hiyo na kutumia kikamilifu huduma zinazotolewa.

“Huduma hizi ni kwa ajili yenu, itumieni hospitali hii ipasavyo badala ya kusafiri mbali kufuata huduma zinazopatikana hapa hapa nyumbani,” alisisitiza Ussi.

Kadhalika, aliwataka wananchi kuendelea kujikinga na maradhi ya Malaria na Ukimwi kwa kuzingatia elimu wanayopewa na wataalamu wa afya ili kulinda afya zao na jamii kwa ujumla.

Akizungumza baada ya kupokea Mwenge wa Uhuru kutoka Wilaya ya Bagamoyo, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Saimoni alisema, Mwenge wa Uhuru mwaka huu unapitia miradi 13 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 10.5.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here