Na Chifu Mussa Bwakila Lukwele IV
IPO methali mashuhuri kwa jamii zote Duniani inayosema “Historia itaendelea kumtukuza muwindaji, hadi Simba atakapojua kuandika” (History will continue to glorify the Hunter, until the Lion knows how to write).
Kimsingi Methali hiyo inabainisha kuwa, wale wenye nguvu za kimamlaka (hasa Wakoloni wetu) ambao wamewakilishwa na “Mwindaji”, hudhibiti Simulizi na Historia (Narratives and History), hadi wale wasio na nguvu (waliokandamizwa / kutawaliwa) ambao wamewakilishwa na “Simba”, waweze kusimulia hadithi zao wenyewe.
Kinachomaanishwa hapa ni jinsi historia inavyoweza kupotoshwa na kuakisi mtazamo pekee wa wale walio na Mamlaka, huku Simulizi ya kweli ikibaki isieleweke au kusahaulika katika tabaka la chini la jaa la historia.
Tunajua kuwa SIMBA ni alama mojawapo ya nguvu, kama ilivyo SUNGURA ni alama ya Ujanja, na FISI ni alama ya UROHO na KUPUMBAA akili; lakini kama SIMBA haitangazi nguvu yake kwa uhalisia wake, basi sifa hiyo itaishia kwake mwenyewe na MUWINDAJI ataendelea kudhibiti Simulizi.
Hivyo, ni muhimu hasa kwa Waafrika (SIMBA) kutoa sauti kwa wasio na sauti ili kuhakikisha uelewa kamili na sahihi wa historia, simulizi na matukio.
Hali halisi:
Historia yetu wenyewe Waafrika imeandikwa na kusimuliwa kiustadi na “MWINDAJI” (yaani Genge lenye nguvu la Waliotutawala kwa Ukoloni Mkongwe, na wanaotutawala sasa kwa ukoloni mamboleo).
Simulizi zetu za Kiafrika juu ya Ustaarabu wa hali ya juu tulionao kabla ya Ukoloni, Elimu, Maarifa na Hekma, sanjari na Maendeleo ya Kimaada havijulikani kutokana na kukandamizwa, na kutengwa; huku mapambano na uzoefu wetu mara nyingi vikipuuzwa hata na wale wanaoitwa Wanazuoni wa Kiafrika wa mawanda ya Historia.
Kwa kuwa historia mara nyingi huandikwa na Mataifa ya Magharibi yanayoiburuza Dunia katika kiza, ni vigumu kupata picha kamili ya hali ilivyokuwa katika kipindi fulani cha maisha yetu au cha wahenga wetu, bila kusikia tafiti za kihistoria na simulizi kutoka pande zote; haswa kutoka kwa wale ambao hadithi zao hazisimuliwi kwa utaratibu wa kawaida (hazipo kwenye mitaala Shuleni au Vyuoni wala kwenye Vitabu).
Bila shaka wengi wamekaririshwa simulizi za Wakoloni Mamboleo kuwa, kabla ya ujio wao (Wazungu), jamii za Kiafrika ikiwemo kwenye eneo hili linaloitwa hivi sasa jina la TANZANIA, wakazi wake walikuwa WAJINGA, wasio na Maarifa yoyote ya kurahisisha maisha yao.
Wanadai kuwa eti kabla ya wao kugawana Afrika ili “waistaarabishe”, Waafrika waliishi kama wanyama wasio na Utawala, Ustaarabu, wala kuwa na lengo la maisha.
Ukweli ni kuwa, tawala zetu ndogondogo za jadi zilizokuwepo kabla ya Ukoloni, zikiwa na mifumo bora ya Utawala, mipaka ya kijiografia ya kila Himaya, Taasisi muhimu za Umma Ulinzi, Usalama, Mahakama, na Mabaraza ya Ushauri (Mabunge).
Na hii ndiyo sababu hadi leo utasikia maneno hasa yanayotumiwa sana na wajamii wa Pwani ya Mashariki mwa Tanzania hasa Waluguru, Wakwere, Wakutu, Wazaramo (n.k) kama vile “MFALME” au “MWINYI” (Mkuu wa Himaya / Mtawala wa nchi); na “MNDEWA” (Mtawala msaidizi).
Vilevile kuna “MZIGIRA” (Waziri); “MSHENGA” (Mkuu kipande kidogo cha nchi chini ya mtawala msaidizi); “MKULU JAKAYA” (Mkuu wa Kaya ambapo kiutawala ndiyo msingi wa Serikali ya jadi) n.k.
Mifumo hii ya utawala inaonesha uwepo wa Elimu ya Uongozi wa Kisiasa na kijamii hadi ngazi ya familia, pia uwepo wa taasisi imara za Haki, pamoja na zile za Haki jinai n.k.
Elimu ya Jadi:
Ikumbukwe kuwa,Elimu ya kabla ya Ukoloni katika eneo la sasa linaloitwa Tanzania, ilikuwa na mundo tofauti sana na wa hivi leo; iliathiriwa na Tamaduni za makabila na Dini, pamoja na maingiliano ya wageni toka Mashariki ya Kati, na Mashariki ya Mbali.
Elimu ya kale ilikuwa mchakato kamili unaotegemea mambo mawili, Mosi jamii, na pili madarasa (shule au vyuo); badala ya mfumo wa sasa unaotegemea zaidi jambo moja pekee yaani madarasa tu (shule vyo pekee).
Mtoto alikuwa wa jamii nzima, hakukuwa na ukomo wa kupata elimu na maarifa (yaani kujifunza kwa binaadamu ukomo wake ni mwisho wa maisha yake).
Elimu ya asili ilizingatiwa sana katika jamii nyingi, ambapo iliunganishwa moja kwa moja na maisha ya kila siku, na miundo asilia ya kijamii.
Mafunzo ya Vitendo yalipewa kipaumbele yakihusishwa moja kwa moja na maisha ya kila siku ya kijamii mathalan maarifa ya uwindaji, uvuvi, kilimo na ufugaji; lakini pia elimu ya ufundi, biashara, malezi, madili, na uongozi.
Mbinu za jumla zilizotumika na makabila mengi ya Tanzania, ni kuhusisha elimu kwa kuwatoa wanajamii kwenye hali duni kiutendaji na kuwapeleka kwenye hali bora zaidi kiutendaji; kwa kushughulikia kila kipengele cha maisha ya kila siku mtu binafsi, jamii na vilivyowazunguuka (mazingira yao).
Walifunzwa juu ya umahiri wa kuwasilisha maarifa, ujuzi wa vitendo, maadili, mwenendo wa kijamii, historia, mila, falsafa ya kila jambo, lugha na Hekima.
Wanajamii, hususan wazee, walikuwa na jukumu kubwa la kufundisha vizazi vichanga vyenye akili nyembamba na upeo mdogo wa ufahamu wa mambo na athari zake, kupitia uchunguzi/utafiti, kuishi kwa kutenda, na kuiga.
Maadili yalipewa kipaumbele kikubwa katika kila aina ya elimu aliyofunzwa mtu, hususan juu heshima kwa wote, ujenzi wa tabia njema, uhusiano na ushirikiano wa kunufaisha kijamii.
Michezo ya jadi, hadithi, methali, nahau, mizungu (mafumbo) michoro na baadae maandishi n.k, vilitumika kama njia muhimu za ufundishaji, na eneo mahususi la kuhifadhia historia ya jamii husika.
Japo Elimu ilitofautiana kulingana na jinsia, lakini wake kwa waume wote walikuwa na haki ya lazima kupata elimu, ujuzi au maarifa kupitia jando, unyago, na matukio maalum kama ya uwindaji, urinaji asali, uvuvi, n.k.
IJAZA (Alama za Kufuzu) zilitolewa kwa Uanafunzi, kupitia hasa mafunzo ya vitendo kama uongozi, ufundi, uvuvi, uwindaji, urinaji asali, kilimo, ufugaji, mbinu za mapigano, Statejia za vita n.k, kwa kufanya kazi chini ya walimu wenye uzoefu zaidi wa taaluma husika.
Wahitimu walipewa IJAZA (alama maalum) baadhi ni alama za kimandishi ikiwemo SHAHADA (baada ya kuja ukoloni hadi hivi sasa vinaitwa “vyeti, Diploma, Digrii ya Kwanza, Digrii ya Uzamili, na Digrii ya Uzamivu”).
Wengine walivalishwa ‘FIA’ (Kofia Maalum ya kutambusha umairi wao kwenye ujuzi au taaluma husika); wapo pia waliovalishwa KILEMBA (rangi zilitambusha ujuzi wao, mfano nyeupe ni elimu ya kawaida, Nyeusi ni elimu ya Uongozi, na Bluu ilionesha kutabahari, kuzamia au kubobea kwenye elimu ya juu/uanazuoni, ambapo baada ya Ukoloni hadi sasa wanaitwa ‘Madaktari wa Falsafa’).
Wengine walipewa vifaa vyenye alama ya ujuzi wao mfano MKUKI, SHOKA, FIMBO n.k.
Wahitimu walifanyiwa sherehe kubwa kutambulishwa kwenye jamii kuwa wamefuzu, japo kufaulu kwao hakumaanishi kuwa hapo ndiyo mwisho wa elimu, bali kujifunza mambo mapya na kupata uzowefu wa wengine, ni suala la lazima hadi mwisho wa maisha ya mtu.
Wapo waliopata Maarifa maalumu (japo elimu zilikuwa kwa manufaa ya jamii nzima, lakini baadhi zilipitishwa kwa watu wachache sana), mfano elimu ya Tiba, na elimu ya Uongozi malum kwa warithi wa Ufalme n.k.
Kwa mitaala iliyoandikwa kabla ya maandishi ya Kirumi, zilitumika Alfabeti za Kiarabu hata kwa kuandikia lugha za kiasili kama Kiluguru, Kishomvi, Kiyao, Kizigua n.k, ambapo hadi sasa kwenye baadhi ya maeneo ya Pwani baadhi ya familia hutumia Alfabeti hizo kuandikia barua za posa.
Kulikuwa na vituo malum (Madarasa / Vyuo) vilivyofunza kuandika, kusoma, kuhesabu, Dini n.k; vituo hivi wakoloni walipokuja waliviita “Bush Schools”, kisha wakavitwaa, na kutambulisha Alfabeti za Kizungu tunazozitumia hadi leo na mitaala yenye muelekeo wa Kimagharibi ikitukuza zaidi uzung (White Supremacy).
Hitimisho:
Japo ipo dhana kuwa jadi na ukale wa Kiafrika havina nafasi kwenye dunia ya sasa ya sayansi na maendeleo, lakini yapo mambo ya kale na jadi yetu yasiyobadilika, mfano Utu, Haki, na Uadilifu; Pia Ustaarabu, Maadili, Ujirani Mwema, Mapenzi, na Kuhurumiana; halkadhalika maisha ya Ushirikiano, Umoja, Amani na Utulivu.
Lililo muhimu ni kukumbatia Historia yetu, utamaduni wetu ambao ndiyo utambulisho wetu, uhai wetu, na utashi wetu, katika maisha yetu ya kila siku; sanjari na KUANDIKA HADITHI ZETU WENYEWE, kwa kupitia kumbukumbu za wahenga (shajara) za masimulizi waliyoyaacha.
Pia, yale ya kurithishana kwa mdomo nayo ni vema tukayatia vitabuni kwa wino wa dhahabu, au njia za kimamboleo kama mifumo ya kielektroniki, filamu, mitandao ya kijamii n.k; hivyo kuweza kurithisha na kuendeleza Elimu, Maarifa, Hekma na Uzowefu wa Wahenga.
Tusipoiandika Historia yetu iliyobeba tunu za Maadili Mema, Umoja, Mshikamano, Amani, Utulivu, Haki, na Uwadilifu, daima itaendelea kumtukuza Mkoloni aliyetutawala ambaye sasa anaendeleza ‘Ubeberu’ na ‘Ukoloni Mamboleo’ kwa Sura ya kile kinachoitwa ‘Haki za Binadamu’ na ‘Demokrasia’.
—
KAMA UNA MAONI, MASWALI, AU USHAURI, KUHUSU MAKALA HII, PIGA SIMU NAMBA +255 788 120690, BARUA PEPE: lukwelepace@gmail.com.