Na Yahya Msangi
HUENDA wengi hawajui visa vya mabwawa ya kufua umeme na historia ya Afrika. Nimeona bora niwaelimishe. Mabwawa haya yana kitu kinaitwa ‘geo-politics’ toka zamani na yapo mabwawa ambayo yamewahi kuhujumiwa ili yasijengwe.
Miongoni mwa mabwawa hayo ni Cahora Bassa (Msumbiji/Afrika Kusini) Aswan (Misri) Akosombo (Ghana), Blue Nile (Ethiopia), Mto Congo (DRC), Jinja (Uganda) na Stiegler’s Gorge (Tanzania).
Kati ya haya mabwawa sita, mawili yalishindikana kujengwa kutokana na ‘geopolitics.’ Bwawa la Mto Kongo na Stiegler’s. Nchini Kongo Patrice Lumumba ambaye alitoa kipaumbele kikubwa na kuonyesha nia thabiti ya kujenga bwawa kubwa kabisa (urefu maili mbili) kukinga maji ya Mto Kongo, aliuawa kikatili na mradi husika ulikwama.
Bwawa lile kama lingefanikiwa kujengwa, lingekidhi mahitaji yote ya umeme Afrika na Ulaya na bado kungekuwa na ziada. Sehemu ambapo bwawa hili lingejengwa, ndio yenye maji mengi na yaendayo kwa kasi zaidi kuliko sehemu nyingine yoyote duniani.
Lumumba angefanikiwa, kusingekuwa na haja ya nchi nyingine yoyote Afrika kujenga bwawa au kununua mitambo ya kufua umeme. Kwa kuzuia ujenzi wa bwawa lile, mabeberu walifanikiwa kuzuia maendeleo ya bara zima la Afrika, kwani kusingekuwa na kijiji au nyumba Afrika ingekosa umeme.
Viwanda vingechomoza mpaka vijijini. Afrika ilizuiwa wakati Ulaya iliyotoka kwenye vita ikiruhusiwa kujenga mabwawa tena ya kuchangia! Sababu kubwa ikipigiwa chapuo ni kuwa, mradi utakuwa na hasara na kwamba, Kongo haikuwa na uwezo kutekeleza mradi ule! Ilipofika zamu ya Stiegler’s hadithi ikabadilishwa.
Si tu kwamba uchumi wa Tanzania haumudu mradi huo (japo Cuba na China walijitolea) ikaingizwa hadithi ya uhifadhi vyura na vipepeo! Eti, itaathiri Selous! Eti, itapunguza watalii. Stiegler’s ikakwama! Sasa Stiegler’s inajengwa, lakini hadithi ni zile zile! Wanaojiita wanaharakati wa mazingira wanadai mradi huo utaathiri Selous, wanadai una gharama kubwa, wanadai kuna viumbe adimu Selous! Yaani chura, popo, vipepeo ni adimu na wana thamani kuliko Watanzania!
Wakati Misri inakusudia kujenga Aswan, Israel akisaidiana na Marekani walikuja juu! Wakamsakama Gamal Abdul Nasser! Lakini, Farao akasimama wima ikajengwa. Akina Israel wakaja Afrika Mashariki kutuambia tukatae, maana watatumia maji yetu! Yani maji ya Ziwa Viktoria na Mto Nile! Wakatuhamasisha tujenge miradi mikubwa ya maji ili yanayoenda Misri yapungue!
Ukweli ni kwamba, maji ya Nile yanazidi mahitaji ya Tanzania, Uganda, Ethiopia, Sudan na Misri. Bado tunatumia chini ya 50% ya maji. Mengi yanaishia Bahari ya Mediterranean ambako hata Israel inanufaika nayo. Hatimaye Nasser akapoteza maisha baada ya kushindwa vitani. Lakini, bwawa la Aswan lipo na ndio msingi wa Maendeleo ya Misri.
Bwawa la Akosombo nalo halikubaki salama. Ni moja ya mambo yaliyowaudhi Waingereza hadi wakasuka mapinduzi ya kumng’oa Kwame Nkurumah. Lakini, mwana wa Afrika alijenga bwawa hilo. Bwawa la Akosombo ndio kiini cha Maendeleo ya Ghana, linauza umeme Togo, Benin, Cameroon na Nigeria!
Cahora Bassa nalo halikumuacha Samora Machel salama! Likitumika kudhoofisha uchumi na harakati za ukombozi Msumbiji. Wakubwa walilipinga! Afrika Kusini ya makaburu ikawezeshwa kujenga vinu vya nyuklia ili bwawa likihujumiwa aumie msumbiji peke yake! Hao hao wakaja kuwanyang’anya vinu vya nyuklia ilipoonekana ANC itatwaa madaraka! Hawataki ngozi nyeusi imiliki nyuklia!
Bwawa la Blue Nile nalo lilipingwa mno! Lakini, Zenawi akafumba masikio. Linajengwa kwa kasi sasa kwa msaada wa China. Ethiopia inasonga mbele kwa kuwa imeongeza umeme. Sasa wana treni ya umeme. Hata nia ya Uganda kujenga bwawa Jinja nayo ilipingwa!
Hii ndio historia ya mabwawa Afrika! Wakubwa hawataki tupate umeme. Wanajua umeme utazalisha Viwanda na tutatumia rasilimali zetu wenyewe. Bahati mbaya, Afrika haina uhaba wa vibaraka! Toka enzi za Lumumba, Nasser, Nkurumah! Mara zote na kote watajitokeza kuwaunga mkono mabeberu. Wanatumia sababu zile zile za enzi za akina Lumumba. Tuwapuuze!