Haya yakifanyika, Wizara ya Maliasili na Utalii itaweka historia

0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Maji Jumaa Aweso wakivuta kitambaa kuashiria uzinduzi wa Mradi wa maji Kigamboni ambao unatoa maji lita Milioni 70 kwa siku kwa ajili ya wakazi wa maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam.

Na Hamis Abeid Baruani

NIANZE kwa kumpongeza Rais wetu kipenzi na Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya na kwa leo kafanya jambo kubwa la kukumbukwa daima kwa Wakazi wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani.

Kwa maisha ya kiumbe hai (binadamu na wanyama) Maji ndio kitu muhimu zaidi maana ndio yanawezesha kila kitu kwenye mzunguko wa maisha ya kila siku, uzinduzi wa mradi wa maji Kigamboni, ni ishara ya kujali utu na ubinadamu kwa Wananchi maana sasa watu wana matumaini ya kupata maji kwa asilimia 100.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiangalia maji baada ya kuwasha mtambo (pampu) wa kutoa maji chini ya ardhi kwenye kisima kirefu (m 450) kwa ajili ya kuyapeleka kwenda kwenye tanki kubwa la maji katika eneo la Kigamboni Jijini Dar es Salaam.

Kwa kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri binadamu na wanyama, na kwa kuwa hili ni janga la dunia linaathiri mazingira kiujumla, tumeshuhudia mbuga zetu na hifadhi nazo zinaathirika na hali hii.

Mito inayopita kwenye mbuga za wanyama na hifadhi zetu mingi imekauka kutokana na uhaba wa mvua hali inayotokana na mabadiliko ya tabia nchi, hivyo kuna umuhimu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa na mpango endelevu na wa dharura wa kuhudumia hii mito.

Hakuna ubishi kwamba, mito hii ndio inayopeleka maji ambayo yanatumika na wanyama kunywa, kukosekana kwa maji kwenye mito hiyo, inasababisha wanyama wafuate maji mbali na pengine kufa kwa ukosefu wa maji na kwa umuhimu zaidi, ikizingatiwa hizi mbuga na hifadhi zinaongeza Pato la Taifa kupitia fedha za kigeni za watalii.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akibonyeza kitufe kuwasha mtambo (pampu) wa kusukuma maji kwenye tanki kubwa la maji kwa ajili ya usambazaji kwa wakazi wa maeneo mbalimbali Jijini Dar es Salaam.

Haya ni maoni yangu kuhusu kupatikana maji kwenye mito mbugani. Kwanza, Wizara ya Maliasili na Utalii iombe sehemu ya mitambo aliyoizindua na kuigawa Rais, iende mbugani na kwenye hifadhi kuangalia sehemu ambazo visima vitachimbwa angalau hata vyenye uwezo wa kutoa maji Lita 500,000 (Laki Tano) kwa kila mbuga.

Maji haya yawe yanatiririshwa kwenye mito hiyo kila siku ili kupunguza ukali wa ukame wa maji ya kunywa kwa wanyama (katikati ya mito yatengenezwe madimbwi ambayo pia maji yatakuwa yanatuwama).

Maji haya yatarahisisha maisha ya wanyama ambao ni sehemu ya utalii, kuwatunza wanyama hawa ni sehemu ya kulinda pato la Taifa.

Pia, jambo la kuzingatia ni kwamba, visima vitakavyochimbwa pembezoni mwa mito huko mbugani, vitakuwa vinatumika kipindi cha ukame tu, mvua zikinyesha basi vinazimwa na kutunzwa; hii itasaidia kulinda maisha ya wanyama kwa vipindi vyote.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akibonyeza kitufe kuzindua Mradi wa maji Kigamboni ambao unatoa maji lita milioni 70 kwa siku kwa ajili ya wakazi wa maeneo mbalimbali katika Jiji la Dar es Salaam kwenye hafla iliyofanyika Kigamboni

Pili, kuanzishwa kwa hifadhi ya chakula cha wanyamapori, hii itasaidia kipindi cha ukame kwa wanyama wanaokula majani na kwa kuwa maisha ya wanyama wanategemeana (ECOSYSTEM), wanyama wanaokula majani wakishiba, wanaokula nyama watawala na watapata nyama nzuri (Swala anakula majani nae analiwa na Simba).

Ninaamini, mambo haya mawili yakifanyika Wizara ya Maliasili na Utalii itakuwa imefanya jambo la kukumbukwa milele na Taifa letu.

*Mwandishi ni Mjumbe Halmashauri Kuu CCM (W) Ubungo anapatikana kwa namba 0683808725

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here