NI nadra nadra sana kupata bahati ya kuaminiwa na Marais wa Awamu Tano kufanya kazi za kiuteuzi katika nafasi za juu.
Mara nyingi kazi za kiuteuzi zinahitaji watu wenye historia nzuri ya kiutumishi, uwajibikaji uadilifu, uvumilivu, uaminifu pamoja na werevu uliotukuka wa kile unachotumwa kwenda kukifanya.
Tanzania inao watu wengi wa aina hiyo, lakini ni wachache waliopata kuaminiwa na Rais au Marais wakamaliza salama utumishi wao kwa heshima ile ile waliyokuwa nao kabla ya uteuzi. Ukosefu wa uadilifu na uwajibikaji sahihi hupelekea wateule wengi kupumzishwa.
Haruna Said Masebu si jina geni kwenye masikio ya Watanzania wanaoishi kuanzia miaka ya themanini tisini hadi sasa.
Mtanzania Haruna Masebu ambaye mbali na kuishi kwa muda mrefu kama mtumishi wa umma, pia ni kada mtiifu na mwaminifu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye kadi ya uanachama wake inasomeka kutoka wilaya ya Urambo, Tabora.
Heshima ya Masebu inabebwa na Kilomita nyingi alizotembea za safari ya maisha iliyompa heshima kubwa ndani ya nchi na Kimataifa.
Mtaalamu huyu aliyezaliwa Machi 6, mwaka 1955 huko Usoke, Wilayani Urambo ni mbobevu katika fani za Uthamini, Uchumi na Uwekezaji kwenye ardhi ambaye amesomea katika Chuo Kikuu cha Reading nchini Uingereza mwaka 1982.
Baada ya kuwa kwenye utumishi kama Mhadhiri na baadae Afisa Mwandamizi katika Wizara ya Ardhi, Masebu alianzishiwa safari mpya ya kiuteuzi baada ya Rais wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi kumteua kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba Taifa (NHC) mnamo mwaka 1994 kazi aliyodumu nayo hadi mwa 1997 huku akiacha mafanikio lukuki kwenye wizara hiyo.
Mojawapo ya fanikio kubwa ni kubwa kuanzia ubia wa watu binafsi na Serikali kwenye miradi ya majengo (PPP). Historia inatueleza kuwa mwaka 1997 Masebu aliitwa kwenda Meneja wa Taasisi ya African Housing Fund Kanda ya Mashariki mwa Afrika akisimamia miradi kwenye nchi 11.
Mwaka 2006 tayari Serikali ya Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ilimuamini mtaalamu huyu na kuteuliwa kuwa mratibu katika Tume ya Rais ya kurekebisha mashrika ya Umma(PSRC) na baadae mwaka huo huo 2006 Rais Kikwete kumteua kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Mafuta (EWURA).
Hakuna Mtanzania asiyefahamu kuwa EWURA ndio imeleta suluhisho kubwa la udhibiti wa bei ya mafuta kwa kuanzisha bei elekezi, ambapo awali kulikuwa na uholela mkubwa uliochangia bidhaa hiyo kuwa chanzo cha mfuko wa bei kwa bidhaa nchini.
EWURA chini ya Haruna Saidi Masebu, imeleta suluhisho kwenye ukaguzi wa ubora wa vituo vya mafuta, bei za maji sambamba na usimamizi wa kuhakikisha wateja wa Maji wanapata huduma bora ikishirikiana na Mamlaka za kikanda za maji nchini.
Masebu alikuwa sehemu pia ya watu walioboresha wazo la Mamlaka ya Nishati Vijijini (REA) kuweka tozo kwenye mafuta yanayosimamiwa na EWURA nia ikiwa ni kuipa REA vyanzo vya uhakika vya mapato.
Masebu ambaye Tanzania haijutii kuwa na mtaalamu wa aina yake, akiwa bado EWURA ndiye alihusika kuanzisha mfumo wa bulk procurement ambapo mfumo huu umewezesha kupunguza bei ya mafuta. Kupitia mfumo huu makampuni mengi sasa yanashiriki biashara ya mafuta. EWURA mkononi kwa Masebu ilipata mafanikio kimataifa na kuwa moja ya taasisi bora duniani
Serikali ya Rais wa Awamu ya Sita chini ya Dkk. Samia Suluhu Hassan iliuona uwezo wake ambapo mwaka huu, 2025 Rais Samia alimteua kwenye tume ya Rais ya Ngorongoro kuangazia changamoto na mafanikio ya zoezi la Uhamaji wa hiari ili kupisha uoto na hifadhi ya wanyama kwenye bonde la Ngorongoro kazi ambayo bado anaendelea nayo sasa hadi muda wa tume utakapomalizika.
Kwa upande wa maendeleo ya jamii, Masebu amekuwa Rais wa Shirika lisilo la kiserikali la Kimataifa linaloitwa SOS CHILDRENS VILLAGES upande wa Tanzania. Shirika au NGO hiyo iko kwenye nchi 137 duniani ikiwemo Tanzania. Taasisi hiyo inajihusisha kusaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu ili waishi na wasome kama vile wako kwenye familia zao.
Masebu bado anazo nguvu akili na mawazo chanya yanayokwenda na kasi ya sasa kwenye kupigania maendeleo ya Taifa kwa mahali popote atakapopewa fursa ya kuaminiwa.
Anaamini katika falsafa ya Rais wa sasa Dkt. Samia Suluhu Hassan inayotengeneza mazingira bora yanayotoa fursa kwa Watanzania wote kushiriki katika kukuza uchumi wa Taifa la Tanzania.