JESHI la Polisi nchini, limetakiwa kuongeza nguvu katika kusimamia utekelezaji wa sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kali zaidi kwa madereva wanaosababisha ajali zinazopelekea vifo.
Agizo hilo limetolewa na Rais wa Jamuhiri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan kupitia salamu zake za pole alizozitoa kufuatia ajali ya barabarani iliyogharimu maisha ya watu 8 na wengine 41 wakijeruhiwa.
Ajali hiyo ya barabarani iliyotokea Alhamisi ya Aprili 3, 2025, ilihusisha basi la abiria ambalo mashuhuda wa tukio wanasema liliacha njia wakati lilipokuwa likipishana na gari dogo na kuangukia korongoni katika Kijiji cha mamba Msangeni wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro.
Basi lililohusika katika ajali hiyo lenye namba za usajili T 222 DNL, mali ya kampuni ya Mvuni, lilikuwa likitoka Ugweno wilayani humo kuelekea Jijini Dar es Salaam.
Katika salamu zake hizo alizozisambaza kwa umma kupitia kurasa zake mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, Rais Samia mbali ya kueleza masikitiko yake kuhusu tukio hilo ametoa wito kwa watumiaji wa barabara kuhakikisha kila mmoja anazingatia kanuni na sheria za usalama barabarani
Kuhusu tabia za madereva ambazo zimekuwa zikielezwa kama chanzo cha matukio mengi ya ajali za namna hii, Rais Samia ameandika akisema;
“Nasisitiza vyombo vyetu vya usalama barabarani kuendelea kusimamia sheria kwa makini ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika, ikiwemo kufuta kabisa leseni kwa madereva wenye makosa yanayochukua uhai wa Watanzania wenzetu”
Kufuatia agizo hilo la Rais, wadau mbalimbali wa usalama barabarani wameeleza kufurahishwa nalo huku wakisema linaweza kuwa muarobaini wa uzembe, kiburi, dharau na ukosefu wa nidhamu ya barabarani kwa baadhi ya madereva.
Akiongea na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu, Habari na Mawasiliano wa Asasi ya Mabalozi wa Usalama Barabarani nchini (RSA Tanzania), Ramadhani Msangi alisema, wanapongeza agizo hilo na wanaamini kuwa, litatekelezwa kwa kuwa kauli ya Rais ni amri.
“Uzuri sheria yetu licha ya mapungufu yake ambayo tunayapigia kelele, inalipa Jeshi la Polisi mamlaka ya kutekeleza agizo hilo la Rais, na tunaamini utekelezaji wake utasaidia kuwaamsha wenzetu ambao wamekuwa wakiendesha magari kwa mazoea badala ya kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani,” alisema Balozi Msangi.
Aliongeza; “Faini zetu zilizoko kwa mujibu wa sheria, zimekuwa hazisaidii sana kuwabadili madereva kitabia, sanasana zimekuwa zikiwapa viburi na dharau kiasi cha kuwafanya mabwana hawaambiliki hata wanapokemewa na madereva kwasababu wanajua hawana cha kupoteza, hivyo adhabu hii naamini itawafanya washikilie na kutembea na akili zao zote.”
Hata hivyo, mwanaharakati huyo wa masuala ya usalama barabarani ametoa wito kwa wanaohusika na mchakato wa kuhuisha mabadiiko ya sheria ya usalama barabarani ambao umekwama toka mwaka 2022 licha ya kuwa muswada wa kwanza wa mabadiliko hayo ulishasomwa Bungeni.
Ajali za barabarani ni miongoni mwa changamoto zinazolikabili taifa letu licha ya juhudia kadhaa ambazo zimekuwa zikifanywa na mamlaka na wadau kama RSA Tanzania za kuelimisha umma wa watumia barabara kubadilika kimtazamo na kimatendo.