UMOJA wa Ulaya (EU) umeahidi kuendelea kuisaidia Tanzania kutimiza lengo la kuwa na maendeleo kwenye sekta ya Uchumi wa Buluu lililoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo (2050) iliyozinduliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Julai 17, 2025.
Hayo yamejiri wakati wa Kikao cha Majadiliano rasmi na Serikali ya Tanzania kuhusu Programu ya Msaada wa kibajeti kupitia Uchumi wa Buluu na Mabadiliko ya Tabianchi kilichofanyika jijini Dodoma Julai 23, 2025.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Mkuu wa Masuala ya Ushirikiano anayeongoza wajumbe kutoka Umoja wa Ulaya (EU) Marc Stalmans alisema wameridhishwa na namna Dira hiyo ilivyoangazia Uchumi wa Buluu hivyo, aliahidi EU kusaidia bajeti katika eneo hilo.
Aidha, alishukuru na kupongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuanzisha Idara inayoshughulika na uratibu wa shughuli za Uchumi wa Buluu ambayo itasaidia kusukuma ajenda ya matumizi ya rasilimali zilipo katika eneo hilo.
Dira 2050 imeweka bayana malengo na shabaha za maendeleo ili kuijenga kujenga Taifa linalohifadhi na kutumia rasilimali za asili kwa ufanisi, uendelevu na tija na linalostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Hivyo, Stalmans alibainisha kuwa kuna kazi ya kufanya katika kuhakikisha programu hiyo kuhusu masuala ya uchumi wa buluu inachukua nafasi na kuleta manufaa kwa wananchi wa Tanzania.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Abdallah Hassan Mitawi aliishukuru EU kwa kuendelea kuisaidia Tanzania katika eneo la Uchumi wa Buluu na kuahidi kuwa Tanzania itatumia ipasavyo misaada itakayotolewa.
Mitawi alisema, kuanzishwa kwa Idara ya Uchumi wa Buluu ni juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha nchi inanufaika na rasilimali hizo.
Alisema sanjari na hilo, kupitia rasilimali hizo, pia maono ya Rais Dkt. Samia katika kufikia lengo la kuendelea kuiwezesha nchi kukua hadi kufikia uchumi wa kati.
Itakumbukwa Sera ya Uchumi wa Buluu ilipitishwa rasmi mwaka 2024 ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais ilipewa jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezaji wa mkakati wake wa mwaka 2024-2034.
Hivyo, Mkakati unatoa mwelekeo wa utekelezaji kwa kuweka mfumo wa ufuatiliaji na tathmini kwa lengo la kuhakikisha Sera ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 inatekelezwa ipasavyo.