MWENYEKITI wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, amezitaka taasisi za serikali na asasi za kiraia kuwaelimisha wananchi kupitia majukwaa mbalimbali juu ya umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa maandalizi ya uchaguzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam, Mwambegele alieleza kuwa Tume inategemea ushirikiano wa wadau katika kuwahamasisha wananchi, hususan wale waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka.
“Wawakilishi wa taasisi na asasi za kiraia mmekuwa mkishirikiana na Tume kwa kuwafikishia wadau taarifa kuhusu michakato mbalimbali ya uchaguzi, ikiwemo zoezi la hivi karibuni la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” alisisitiza.
Aidha, alibainisha kuwa Tume imeshatangaza ratiba ya uchaguzi huo kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa chini ya Ibara ya 41(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 49(1)(a) na 68(1) vya Sheria ya Uchaguzi Na.1 ya mwaka 2024.
Kwa upande wake, Elias Mtinda, Meneja wa Programu kutoka taasisi ya ActionAid, aliipongeza Tume kwa kuandaa mkutano huo akibainisha kuwa taasisi zisizo za kiserikali zina mchango mkubwa katika kutoa elimu kwa wapiga kura, hasa kwa vijana na wanawake waliopo vijijini.
Hata hivyo, alieleza changamoto ya kufikia maeneo ya vijijini ambayo yako mbali na miji, hali inayokwamisha utoaji wa elimu kwa wakati.
Mkutano huo unajumuisha wawakilishi wa taasisi za serikali, asasi za kiraia, wahariri na waandishi wa habari, na unatarajiwa kufikia kilele chake Agosti 4, 2025.
Kaulimbiu ya mkutano ni: “Kura yako, Haki yako – Jitokeze Kupiga Kura.”