Dkt. Samia aahidi kukuza sekta ya utalii na michezo Arusha

0

MGOMBEA wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. 𝗦𝗮𝗺𝗶𝗮 𝗦𝘂𝗹𝘂𝗵𝘂 𝗛𝗮𝘀𝘀𝗮𝗻, amesema, dhamira yake ni kuendelea kuimarisha na kukuza sekta ya utalii mkoani Arusha na nchi kwa ujumla kwa kuboresha vivutio, kuongeza miundombinu na kukuza utalii wa michezo.

Dkt. Samia ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha, Oktoba 2, 2025.

Akihutubia maelfu ya wananchi hao, Dkt. Samia amesema tayari serikali imepanua na kuboresha kiwanja cha Ndege cha Arusha ambacho kuanzia Januari 2026 kitaanza kufanya kazi usiku na mchana na kubainisha kuwa hatua hiyo itachochea moja kwa moja ukuaji wa biashara, kurahisisha usafiri na kuongeza idadi ya watalii.

Aidha, akitoa ahadi zake katika miaka mitano ijayo, Dkt. Samia ameahidi kujenga Ukumbi mpya wa Kimataifa wa Mikutano wenye uwezo wa kuhudumia watu 6,000 kwa wakati mmoja pamoja na hoteli na huduma zingine, sambamba na kituo cha urithi wa kijiolojia katika eneo la Ngorongoro Lengai kitakachovutia wanasayansi na watalii wenye nia ya kujifunza historia, ikolojia na masuala ya kisayansi.

Akigusia kuhusu sekta ya michezo, Dkt. Samia amesema, iwapo atachagulia basi serikali yake itahakikisha ujenzi wa uwanja wa michezo wa AFCON unaoendelea Jijini Arusha unakamilika ifikapo Julai 2026 na kuanza kutumika.

Vilevile, amebainisha kuwa ukamilishwaji wa ujenzi wa uwanja huo ambao ujenzi wake umefikia asilimia 63, utaenda sambamba na mradi wa Mji wa AFCON katika eneo la Bondeni City, utakaokuwa kivutio kipya kwa wageni na watalii.

Huu ni muendelezo wa mikutano ya kampeni za Urais kupitia CCM ndani ya mkoa wa Arusha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here