Dkt. Mwinyi: Tutatoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu

0

MGOMBEA wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu kwa kuwajumuisha kikamilifu katika maeneo ya uongozi, ajira, elimu na huduma nyingine muhimu, kupitia Sera ya Uwezeshaji.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, Oktoba 15, 2025, alipokutana na makundi ya watu wenye ulemavu katika hafla ya kampeni zake iliyofanyika katika Ukumbi wa Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema Serikali inalenga kushirikiana kwa karibu na watu wenye ulemavu, ikiwa ni pamoja na kuwaongezea nafasi katika vyombo vya maamuzi kama Baraza la Wawakilishi, sambamba na kuzingatia ushiriki wao katika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini.

Aidha, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaweka mgao maalum wa fedha kwa ajili ya watu wenye ulemavu, sambamba na kutoa mafunzo ya kuwawezesha kuendesha shughuli zao za kiuchumi kwa ufanisi.

Amesisitiza kuwa mikopo ya masharti nafuu itaongezwa kupitia mifuko ya uwezeshaji ili kuwawezesha kufanikisha malengo yao ya kujitegemea.

Kuhusu miundombinu, Dkt. Mwinyi ameahidi kuwa Serikali itaweka mpango wa kuwapatia watu wenye ulemavu maeneo maalum ya kufanyia biashara katika masoko mapya yanayojengwa, pamoja na kuhakikisha majengo yote mapya yanakuwa na miundombinu rafiki kwa watu wa makundi yote maalum.

Akiangazia masuala ya afya na ustawi, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaondoa ushuru kwa vifaa visaidizi vya watu wenye ulemavu vinavyoingizwa nchini ili kushusha bei ya vifaa hivyo, na itaendelea kuwapatia vifaa hivyo bila malipo.

Halikadhalika, ametangaza mpango wa kuanzisha kituo maalum (One Stop Center) cha huduma za matibabu kwa ajili ya watu wenye ulemavu ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa haraka na kwa ufanisi.

Katika upande wa michezo, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaielekeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo kuandaa utaratibu utakaowawezesha watu wenye ulemavu kutumia viwanja vya michezo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here