RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inahitaji wawekezaji watakaowekeza katika miradi itakayowanufaisha wananchi moja kwa moja, kuinua ustawi wao na kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya nchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipofungua rasmi Diko la Mazizini, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ameeleza kuwa Zanzibar bado ina fursa kubwa za uwekezaji, na kwamba Serikali inahamasisha wawekezaji kuwekeza katika miradi ambayo, pamoja na kuwaletea faida wao wenyewe, pia inatoa ajira, fursa za biashara na kuongeza kipato cha wananchi kupitia miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.
Hafla hiyo pia iliambatana na ufunguzi wa Msikiti wa Masjid Hussein Ali Mwinyi, ambao pamoja na Diko la Mazizini, umejengwa chini ya ufadhili wa Mwekezaji Naadhim Alrahman kutoka Oman, kwa gharama ya Dola za Marekani 400,000.
Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kufurahishwa na kazi nzuri iliyofanywa na mwekezaji huyo, akibainisha kuwa uwekezaji huo umeibadilisha mandhari ya eneo la Mazizini, na kuweka mazingira bora kwa wavuvi na wananchi kufanya biashara pamoja na shughuli zao za uvuvi kwa ufanisi zaidi.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewasisitiza wananchi kuyatunza majengo hayo kwa kuzingatia usafi na mazingira bora, ili yadumu katika hali nzuri wakati wote.
Ameukabidhi Msikiti wa Masjid Hussein Ali Mwinyi kwa Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, na Diko la Mazizini kwa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kwa ajili ya usimamizi.