MGOMBEA wa kiti cha Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa CCM imejipanga kumaliza changamoto ya ajira kwa vijana endapo atachaguliwa kuendelea kuongoza katika Awamu ya Pili ya uongozi wake.

Rais Dkt. Mwinyi aliyasema hayo alipokutana na makundi ya bodaboda, wakulima wa mazao ya viungo na wajasiriamali wa Shehia ya Mndo, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Ameeleza kuwa, Serikali ijayo itaendelea kutoa ajira kwa vijana wenye sifa katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya na nyenginezo, sambamba na kuwawezesha kwa mafunzo ili kujiajiri wenyewe.
Aidha, amesema kuwa kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA), Serikali itaendeleza programu za mafunzo, utoaji wa mitaji, maandalizi ya masoko, upatikanaji wa vitendea kazi pamoja na kuboresha mazingira ya wajasiriamali.

Akizungumzia kilimo cha mazao ya viungo, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itatenga maeneo maalum kwa ajili ya kilimo hicho na kuwapatia wakulima pembejeo, mbolea na masoko ya uhakika.
Vile vile, Serikali imekusudia kutoa mitaji midogo kwa wajasiriamali ili waweze kujikwamua kimaisha, pamoja na kuwawezesha waendesha bodaboda kupata vitendea kazi kupitia mikopo itakayotolewa kwa vikundi vya ushirika watakavyoanzisha.

Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa Serikali inajipanga kutafuta fedha za kutosha ili kuwawezesha wajasiriamali wengi zaidi.
Amewataka wananchi kukichagua Chama Cha Mapinduzi kwani ndicho chama pekee chenye uwezo wa kudumisha amani na kuleta maendeleo nchini.