MGOMBEA wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuunda Tume Maalum itakayofanya tathmini ya kina kuhusu fidia walizolipwa wananchi waliopisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo ya Fumba, Nyamanzi, Dimani na Bweleo, ili kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake stahiki.
Dkt. Mwinyi amesema Tume hiyo itapitia na kuhakiki fidia zote zilizolipwa kwa wananchi kwa lengo la kujiridhisha kuwa kila anayestahiki amelipwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
Ametoa ahadi hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Michezo, Dimani, Mkoa wa Mjini Magharibi leo Oktoba 14, 2025, ambapo wananchi wengi walieleza kutoridhika na fidia walizopokea baada ya kupisha miradi ya uwekezaji na maendeleo katika maeneo yao.
Rais Dkt. Mwinyi amewataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kudhibiti udanganyifu unaofanywa na baadhi ya watu wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo kujenga haraka au kuotesha miti kwa lengo la kudai fidia, jambo ambalo halikubaliki kisheria.
Aidha, amewahakikishia wananchi kuwa Serikali na yeye binafsi hawataridhia mtu yeyote kudhulumiwa, na kila anayestahiki atalipwa fidia yake kwa mujibu wa eneo analomiliki. Amesema lengo la Serikali ni kuwaondoa wananchi katika umasikini, si kuwatia umasikini.
Halikadhalika, Dkt. Mwinyi ameagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Masheha kuhakikisha wananchi wanapatiwa elimu kabla ya kutekelezwa kwa miradi yoyote ya maendeleo, sambamba na kupiga picha za maeneo husika ili kuweka kumbukumbu sahihi zitakazosaidia kuepusha migogoro ya ardhi.
Ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kumpa ridhaa ya kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa awamu nyingine, ili aweze kukamilisha utekelezaji wa ahadi zake na kuleta maendeleo makubwa zaidi kwa wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Muhammed Said Dimwa, amesema Chama hakikukosea kumteua Dkt. Mwinyi kuwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar.