Dkt. Hassan Abbas avutiwa na ubunifu wa TFS katika Utalii wa Kidijitali

0

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, amepongeza ubunifu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), hususan matumizi ya teknolojia ya kidijitali kupitia mfumo wa e-Misitu App, ambao unaimarisha huduma kwa watalii na wananchi.

Akizungumza Juni 18, 2025, alipotembelea banda la TFS katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Dkt. Abbas alisema mfumo huo ni mfano bora wa mageuzi ya kidijitali yanayopaswa kuigwa na taasisi zote za serikali.

“Napongeza sana TFS kwa ubunifu, hasa huu wa utalii ikolojia kupitia mfumo wa e-Misitu. Natamani taasisi zote ziwe na mifumo ya namna hii, na muhimu zaidi, mifumo hiyo isomeane ili kurahisisha huduma kwa watalii,” alisema Dkt. Abbas.

e-Misitu App ni mfumo wa kidijitali uliobuniwa na TFS ili kuwawezesha watalii kupanga na kulipia huduma katika hifadhi za misitu kwa njia rahisi, salama na ya moja kwa moja.

Kupitia mfumo huo, watumiaji wanaweza kuona vivutio mbalimbali vya ikolojia, kufuatilia matukio ya burudani, michezo na mila yanayofanyika ndani ya hifadhi hizo.

Dkt. Abbas pia amepongeza ubunifu wa TFS kwa kuanza kutumia viwanja vya michezo kama jukwaa la kutangaza vivutio vya misitu, akisema hatua hiyo inaongeza uelewa wa umma kuhusu utalii wa ndani.

“Nimefurahi kuona matangazo ya TFS kwenye viwanja vya michezo. Watu wanaangalia Azam TV au wakiwa uwanjani wanaona vivutio vyetu vya misitu. Hii ni njia nzuri sana ya kuhamasisha utalii wa ndani,” aliongeza.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa TFS, Harold Chipanha, alisema taasisi hiyo imepokea na kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu kuongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika taasisi za umma.

“Kaulimbiu ya mwaka huu ni maono ya Rais. Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo na sisi wasaidizi wake tumeipokea kwa uzito mkubwa. Kazi yetu ni kuyatafsiri maelekezo hayo na kuyaweka kwenye matendo,” alisema Chipanha.

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2025 yameanza rasmi Juni 16, 2025 na yanatarajiwa kufikia kilele chake Juni 23, 2025. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Himiza matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here