Dkt. Chana atumia uzinduzi wa filamu ya ‘Tantalizing Tanzania’ kunadi vivutio vya utalii

0

Na Happiness Shayo, India

FILAMU ya kutangaza vivutio vya utalii vya nchini Tanzania ijulikanayo kama “Tantalizing Tanzania” inayomhusisha mwanamuziki wa India Shakti Mohan aliyepiga picha mjongeo katika hifadhi za Serengeti, Ngorongoro na Zanzibar imezinduliwa Desemba 13, Mumbai nchini India.

Filamu hiyo iliyoandaliwa na Kampuni ya Swahili iliyopo Mumbai nchini India imezinduliwa rasmi na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga.

Uzinduzi huo uliratibiwa na Kampuni inayohudumia watalii nchini India na Tanzania ya Swahili Safari kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini India.

“Mafanikio ya jitihada zetu yanaakisiwa katika takwimu za Barometer ya Utalii ya Umoja wa Mataifa, iliyochapishwa Januari 2024 inaonyesha kuwa, mwaka 2023, Tanzania ilikaribisha watalii milioni 1.8 waliovunja rekodi, ikiwa ni ongezeko kubwa la asilimia 24.3% ukilinganisha na mwaka 2022 sambamba na ongezeko la mapato yatokanayo na utalii takribani dola za Kimarekani bilioni 3.4, jambo linaloonyesha uthabiti na ukuaji wa sekta ya utalii nchini Tanzania” Chana alifafanua.

Alisema, kupitia filamu ya “Tantalizing Tanzania” inawakilisha maendeleo makubwa katika kuongeza ufahamu wa Tanzania kama kivutio cha utalii nchini India, na kwamba filamu hiyo itaongeza idadi ya watalii kutoka nchini India, jumla ya 44,438 mwaka 2023.

Chana ametumia fursa hiyo kunadi vivutio vya utalii huku akisisitiza Tanzania imejaliwa kuwa na maliasili, vivutio vya kuvutia vya kiutamaduni, na fukwe za bahari za bara na Zanzibar zinazotoa fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kuendeleza huduma za malazi katika maeneo ya hifadhi na maeneo ya mijini, kuimarisha utalii wa fukwe kwa kuanzisha hoteli za fukwe na kupanua huduma za burudani na burudani.

Kwa upande wake Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga amepongeza waandaaji wa Filamu hiyo kwa kuwa imeakisi uhalisia wa vivutio vilivyoko Tanzania Bara na Zanzibar na kusema kuwa, huo ni mwendelezo wa mikakati ya kuvutia watalii nchini Tanzania.

Naye, Mkurugenzi wa Swahili Safaris India, Rajiv Jagat Desai, alisema filamu hiyo imelenga kuonyesha Tanzania kama nchi ya kipekee yenye Utalii wa wanyamapori katika Hifadhi za Taifa pamoja na fukwe na mwaka 2024 imefanikiwa kupeleka watalii 100 nchini Tanzania.

“Tumeamua kama tunataka kuitangaza Tanzania ni lazima kumtumia msanii kuja nchini tanzania ili avutie watalii wa India hivyo watu wa India wataijua vizuri zaidi Tanzania” alisisitiza.

Uzinduzi huo umehudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini India, Anisa Mbega, Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania, Balozi Dkt. Ramadhani Dau, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania, Ephraim Mafuru, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Arif Abbas Manji, Mwakilishi kutoka Shirika la Ndege la ATCL, Wakurugenzi wa Kampuni ya Swahili Safari India na baadhi ya wananchi kutoka Mumbai India.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here