Dkt. Biteko aeleza Mapinduzi yaliyofanywa na Serikali sekta ya elimu

0

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

SERIKALI imeendelea kutambua mchango wa walimu katika maendeleo ya sekta ya elimu kwani ni wazalishaji wa watalaamu mbalimbali waliopo katika sekta zote ikiwemo afya, nishati, sayansi na teknolojia. Sambamba na kufanya maboresho yatakayowaongezea walimu ari ya kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu na kutanguliza mbele maslahi ya Taifa.

Mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo yanachangiwa moja kwa moja na walimu. Hivyo, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kina mchango mkubwa kwa jamii na kwa Taifa kwa ujumla kwa kuwa pamoja na jukumu la kufundisha na kujengea watu maarifa, mwalimu ni mzazi wa kiroho, kiongozi wa fikra, na ni mjenzi wa maadili katika jamii.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko Juni 8, 2025 jijini Dodoma wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Saba wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT).

Alisema, katika kuimarisha sekta ya elimu ili kuongeza ufanisi na kusogeza huduma kwa jamii. Serikali imefanikiwa kujenga jumla ya madarasa 62,685 kwa shule za msingi na sekondari, shule mapya za sekondari 1,031, shule mpya za msingi 1,580 na nyumba za walimu 1,792.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2024/25, Serikali imefanikiwa kuwalipa malimbikizo ya mishahara walimu 101,596, kulipa watumishi 156,556 madeni yasiyo ya mishahara na kuongeza mshahara kwa watumishi wa umma ambapo kima cha chini kuanzia mwezi Julai, 2025 kitakuwa shilini 500,000 badala ya 370,000.

“Serikali inaendelea kutoa ajira za walimu ambapo kuanzia mwaka 2021 hadi sasa, jumla ya walimu 40,527 wameajiriwa katika maeneo mbalimbali nchini. Lengo la kufanya hivi ni kutatua changamoto mbalimbali zilizopo,” alisema Dkt. Biteko.

Amepongeza matokeo ya zoezi la ‘Samia Teachers Mobile Clinic’ kwa kuwafikia walimu 48,380 pamoja na kutatua kero zao huku akiwaomba kuongeza ubunifu utakaowawezesha kuwa na mikakati mingine yenye lengo la kuimarisha utendaji katika sekta ya elimu na kushirikiana na Serikali kwa kutekeleza miradi ya Elimu ya TEHAMA kwa walimu na miradi mingine isambae kwenye mikoa yote nchini.

Kuhusu ombi la walimu kuwa na mwajiri mmoja anayeshughulikia masuala yote ya walimu ili kuimarisha ufanisi katika kuwasimamia, Dkt. Biteko alisema Serikali imelipokea ombi hilo na italifanyia tathmini ili kubaini endapo utaratibu uliopo sasa una changamoto zinazolazimu kutatuliwa kwa kuanzisha chombo kitakachosimamia walimu wote nchini.

Amezungumzia utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa na kusema kuwa lengo lake ni kukuza elimu inayotolewa nchini na kuwafanya wanafunzi waweze kujitegemea wanapomaliza masomo yao. Aidha, Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa walimu wote wanapata mafunzo ili waweze kuendana na mabadiliko hayo.

Fauka ya hayo, kufuatia kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa CWT, amewasihi wajumbe wa Mkutano huo kutumia haki yao katika kuchagua viongozi watakaowaongoza vyema na kuwataletea maendeleo pamoja wagombea kuomba kura kwa heshimiana.

“Nawasihi kuendelea kusimamia misingi ya haki, usawa na uwazi hususan wakati wa majadiliano na utatuzi wa masuala yote yanayohusu chama chenu. Niwaombe watakaoshinda msiwanange watakaoshindwa na mtakaokosa nafasi msikasirike, asitokee mtu wa kuwagawanya, msigawanyike hii ni taalamu ya pili ya uumbaji, mshikamane, mpendane na mshirikiane,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwan Kikwete amesema kuwa Serikali inathamini mchango wa walimu katika mipango mbalimbali ya Taifa na kuahidi kuendeleza ushirikiano mzuri kwa ajili ya ujenzi wa Taifa na uchumi imara.

Kupitia mkutano huo, Rais wa Chama Cha Walimu Tanzania, Leah Ulaya amempongeza Rais Samia kwa utendaji kazi wake na kuahidi kuwa CWT itaendelea kushirikiana na Serikali .

Naye, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Joseph Misalaba ameishukuru Serikali kwa kuendelea kulipa stahiki mbalimbali za walimu ambapo walimu wamenufaika kwa kupandishwa vyeo, ulipwaji wa malimbikizo ya mishahara na madeni yasiyo ya mishahara.

“ Kwa niaba ya watumishi wa Tanzania hususan walimu wote tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kusikiliza kilio cha wafanyakazi juu ya suala la kikokotoo cha mafao ya kustaafu na kuridhia kuboresha kikokotoo kutoka asilimia 33 hadi asilimia 40.

Chama cha Walimu Tanzania kinaiomba Serikali yako iendelee kufanya maboresho zaidi ili kuleta ustawi wa walimu wetu wastaafu ambao wameitumikia nchi yao kwa uaminifu mkubwa,” alisema Misalaba.

Amefafanua kuwa CWT ni chama cha wafanyakazi ambacho msingi wake mkubwa ni kutetea haki na maslahi ya wanachama wake. Kama mdau wa elimu CWT itaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wa elimu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu nchini.

Aidha, Mkutano huo wa mwaka wa CWT umehudhuriwa pia na wawakilishi wa vyama vya walimu kutoka nchi za Rwanda, Burundi, Afrika Kusini na Namibia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here