Na Mwandishi Wetu
IBARA ya 16 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, inatoa haki ya ulinzi wa faragha kwa kila Mtanzania.
Ndio maana, kwa kutambua umuhimu huo, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliridhia utungwaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Namba 11 ya mwaka 2022.
Mara baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo, ikaundwa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), ambacho ni chombo huru cha udhibiti kinachosimamia na kutekeleza Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini.
Tume hii ilianzishwa rasmi Mei 1, 2023, ambapo ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo. Pili, ina jukumu la kufanya tafiti na kufuatilia maendeleo ya teknolojia yanayoathiri usalama wa taarifa binafsi.
Tatu, PDPC ina jukumu la kuwasimamia wakusanyaji na wachakataji wa taarifa binafsi. Nne, kupokea, kuchunguza na kushughulikia malalamiko yanayohusiana na ukiukwaji wa haki za faragha.
“Nina uhakika, hakuna ambaye angependa faragha zake zitolewe hadharani, maisha ni drama (maigizo) kwa hiyo kuna yale mambo ambayo unayafanya ‘behind the scene’ na mengine jukwaani, huo ni uhuru wako na faragha zako,”
“Unadhani ningependa kila mtu ajue ninayoyafanya behind the scene? Huo ndio utu wangu, kama hivi tunavyoongea, tunaongea kila mtu akiwa na utu wake, kwahiyo mnaweza kuona umuhimu wa jambo hili tunaloliongelea, sisi wenyewe na watu wengine,” anasema Mkurugenzi Mkuu wa PDPC Emmanuel Lameck Mkilia.
Mkilia amesema hayo wakati akizungumza kwenye Warsha iliyoandaliwa na tume hiyo kwa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, kupitia Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), iliyofanyika Machi 1, 2025, Mjini Morogoro.
Anasema, waandishi wa habari hususani wahariri, ni nyenzo muhimu ya kufikisha ujumbe kwa jamii, ndio maana wakaamua kukutana nao, ikizingatiwa PDPC sehemu kubwa ya kazi zao ni kutoa elimu kwa umma.
“Kwahiyo, sisi tume ya ulinzi wa taarifa binafsi, sehemu kubwa ya kazi yetu ni elimu kwa umma, basi tunaamini kwamba silaha yetu kubwa ni kuhakikisha jamii nzima inaelewa umuhimu wa kulinda faragha hasa katika dunia hii ya Kidigitali ambayo taarifa zinasambaa kwa haraka,” anasema.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, miongoni mwa taarifa ambazo zinapaswa kulindwa ni jina kamili, kabila, jinsia, elimu, anuani, namba ya simu, barua pepe (e-mail), taarifa za kifedha au afya, namba ya hati ya kusafiria (pasipoti) na taarifa nyingine ambazo ukiziona au kuzisikia, zinakupa nafasi ya kumjua/kumtambua mtu.
“Kila binadamu ana faragha, na hiyo ndio tunayoilinda katika dunia ya teknolojia ambapo taarifa binafsi zinaweza kusambazwa kwa haraka zaidi kuliko zamani, tulinde haki zetu, ni haki za kibinadamu. Hakuna ambaye angependa kuona taarifa zake za kiafya ziko kwenye magazeti,” anasema Mkilia.
Anasema, pamoja na umuhimu wake, suala la kupitishwa kwa sheria hiyo na kuundwa kwa PDPC haikuwa kazi rahisi na ilichukua muda kabla ya kufanyika maamuzi; hiyo ilichangiwa na mitazamo tofauti ya waliopata nafasi ya kulijadili jambo hilo.
“Mnaweza kuangalia na kuona sheria hii ilichukua miaka kumi kuamua kama tunaihitaji au hatuihitaji, kwamba ni jambo la muhimu, lakini wengine waliliangalia kwa mtazamo wa kisiasa.”
Aliendelea kusema: “wengine waliliangalia kwa mtazamo mwingine kwamba, mtu mmoja ndio tumkabidhi faragha zetu? Lakini kumbe, sheria inawataka watu wote watakaotoa huduma kwa njia za Kidigitali, ili wakuhudumie ni lazima utambue jina lako lipo pale,”
“Kwahiyo sheria hii inawataka taarifa zako wazilinde. Tunachokilenga ni lazima uridhie, huo ndio utu na huo ndio ubinadamu, na huo ndio utu wetu ambao tunatakiwa kuulinda.”
“Mfano tuchukulie madhara ya wizi wa utambulisho uliofanywa na mtu mmoja aliyeiba taarifa za fedha za watu wengi mitandaoni, unaweza kusababisha watu wengi kuibiwa fedha zao au kupoteza fedha nyingi.”
“Tunaweza tusilione hili kama ni tatizo kubwa, lakini kwa Tanzania hivisasa bado tupo kwenye kujenga teknolojia ambayo itatuwezesha kupata huduma za kimtandao vizuri zaidi,”
“Tunaongelea tuna Mamlaka ya utambulisho na tunahitaji utambulisho, na Rais alisema anataka kila Mtanzania atambuliwe tena Kidigitali, hiyo ina faida kubwa sana kwenye uchumi wa Kidigitali,” anasema Mkilia.
Aidha, Mkilia anasema mtu akitambuliwa, kila kitu kitakachofanyika Kidigitali, kinamaanisha huyo mtu, “kwasasa utaulizwa naomba kitambulisho cha mpigakura, leseni ya udereva, kitambulisho cha NIDA, lakini utakuta katika vitambulisho vyote, majina yanaweza kuwa tofauti tofauti.”
“Tunapozungumzia wizi wa utambulisho, kila kitu nikatachokifanya, nitafanya na gharama zote zitakuja kwako, kwahiyo tunapoliongelea suala hili, utaona tunaliongelea kwa ukubwa wa kiasi gani,” anasema.
Akielezea zaidi dhana hiyo ya ulinzi wa taarifa binafsi Mkilia anasema, inamuhusu kila mtu na kama jamii itashindwa kuielewa, itaishi kwa mizozo ya kisheria kama ilivyotokea kwenye nchi kadhaa, ambapo kampuni kubwa zilipata hasara kutokana uvujaji wa taarifa binafsi za watu.
“Kutokuelewa dhana hii, kunaweza kuwa na athari sio tu kwa mtu binafsi, bali kwa jamii nzima na hata uchumi na ulinzi wa Taifa letu. Ulinzi wa taarifa binafsi unasaidia kudhibiti wizi, unyanyasaji, unyanyapaa kwenye jamii,” anasisitiza.
Anasema, pamoja na kwamba suala hili linagusa utu, lakini pia linaangalia usalama wa nchi, maana adui akishajua taarifa binafsi, ni rahisi zaidi akajua namna gani anaweza kuwatawala au kufanya chochote.
Hata hivyo, Mkilia kupitia jukwaa hilo anasema, katika kutekeleza majukumu yao, wanakabiliwa na changamoto ya utamaduni na aina ya uhandishi hususani katika zama hizi za Kidigitali, na kuwasihi wahariri kuangalia namna ya kufanya mabadiliko ya uhandishi.
Mkurugenzi huyo anasema, hivisasa kuna ongezeko kubwa la matumizi ya taarifa binafsi kwenye habari zinazotolewa kwenye vyombo vya habari na kuwataka waandishi kutafakari kabla ya kutoa habari husika na kujiuliza hii taarifa ninayoitoa itamfurahisha huyo ninayemuandika?
Anasema, katika zama hizi za kukua kwa teknolojia, taarifa zinasambaa kwa muda mfupi na zinaweza kuleta madhara kwa mtu katika kipindi chote cha maisha yake, “Kwasababu teknolojia tunayo, na teknolojia ipo kwa ajili ya kurahisisha na kuhakikisha tunapata huduma kwa wakati,”
“Lakini tunapoongelea kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi, tunaongelea taarifa za msingi, ni utu na ndio zinazosababisha tuonekane kama tulivyo. Hakuna ambaye angependa siri zake, faragha zake zianikwe,” anasisitiza Mkilia.
Wakitoa maoni yao, baadhi ya wahariri wanasema, kupitishwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na kuundwa kwa PDPC, kunaonyesha wazi Rais Samia Suluhu Hassan anavyoheshimu utu na ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha faragha za watanzania zinalindwa.