Demokrasia ya kweli hujengwa kwa hoja, si kwa makelele

0

Na Mwandishi Wetu

WAKATI mdomo unapopewa ulimwengu katika zama hizi za mabadiliko ya kisiasa na kijamii, dhana ya uhuru wa kuongea (freedom of expression) imewekwa kama alama ya heshima kwa nchi zinazojinasibu kuwa za kidemokrasia.

Hii ni nguzo mojawapo kuu katika Katiba nyingi duniani, ikitambuliwa kama haki ya msingi ya binadamu. Je, uhuru huu una mipaka? Je, unaweza kubeba sumu iliyofichwa ndani ya dhahabu ya maneno?

Je, kuna uwezekano kuwa tunaitukuza sauti zetu huku tukizika misingi ya utulivu, heshima, na maadili ya pamoja? Hali hii inazua tafakuri, kuhusu namna tunavyotafsiri demokrasia na hasa kipengele hiki kinachojulikana kama uhuru wa kuongea.

Katika baadhi ya nchi, demokrasia imegeuka kuwa jukwaa la kelele zisizo na mwelekeo. Kila mtu anasimama kuzungumza; si kwa hoja bali kwa hisia. Maneno yamekuwa mikuki. Tusi limegeuka hoja ya kisiasa. Kejeli zimegeuka sera sehemu mbalimbali za kisiasa.

Katika muktadha huu, uhuru wa kuongea umekuwa msumari wa jeneza la utulivu wa kijamii kwenye Mitandao. Wanasiasa sasa wanapanda chuki, dhihaka, na huzuni kama mbegu za kisiasa kwa kutumia uhuru huu.

Wanatamka maneno yanayogusa hisia za watu maskini, waliochoka na mfumo, lakini suluhisho halitolewi. Wanaishia kuwa watu wa propaganda na si sera.

Hii ndio tabia ya demokrasia ya karne ya 21. Mtu anasimama jukwaani, anawateka watu kwa maneno, anawahadaa kuwa yeye ni mkombozi, kisha anawaachia yale ya msingi kama uchumi, maadili, na mshikamano wa Kitaifa.

Tukiachana na nadharia, tujiulize kwa uhalisia. Je, uhuru wa kuongea unaweza kuleta madarasa kwenye shule za kijijini kwenu? Je, matusi ya kisiasa mitandaoni yanaweza kujenga hospitali kijijini Kwenu? Je, dhihaka za wanaharakati kwenye majukwaa zinaweza kuziba mashimo barabarani kijijini kwenu?

Je, kejeli kwa viongozi zitaajiri vijana walio mitaani? Jibu ni hapana. Maneno hayawezi kuchukua nafasi ya sera. Kejeli hazibadilishi maisha ya watu. Uhamasishaji wa kisiasa wa mitandaoni hauwezi kubeba, bila ujenzi wa taasisi, nidhamu ya kiutendaji na uongozi thabiti.

Kwa kusema hivyo sina maana uhuru wa kuongea usiwepo, una umuhinu wake, lakini Kwa upande mwingine, Uhuru wa kuongea ni muhimu, lakini kama hauna mipaka ya kiitikadi, kiakili, na kitabia, hugeuka kuwa silaha ya kuharibu.

Inapofika hatua ambapo mtu anaweza kutukana Mamlaka na akapata watetezi! Inafikirisha kidogo, Kiongozi wa Dini anatukanwa au naye anashiriki kutukana; hii inatufikirisha, au hata mtu wa kawaida tu anatamka siri za ndani ya Mamlaka au zinazofanania hadharani bila hofu ya kuchukuliwa hatua. Hii sio sawa!

Hapo jamii inakuwa kwenye hatari ya kuvunjika kwa mfumo wa heshima, nidhamu, taratibu na sheria. Ndio hawa hawa ambao hatua zikichukuliwa hukumu za (freedom of expression) kule mitandaoni zinatoka kwa kasi kwelikweli, hapana haya yatufikirishe.

Katika mazingira haya, demokrasia haijengi bali inabomoa. Inapunguza heshima kwa taasisi. Inadhoofisha sheria kwa kisingizio cha “kuongea kwa uhuru”. Serikali inashambuliwa si kwa hoja bali kwa hisia. Wananchi wanapotoshwa na propaganda badala ya mwelekeo wa maendeleo.

Aidha, utandawazi umekuja na sauti nyingi. Wapo wanaosema, “Free speech is a pillar of civilization,” lakini hawasemi kuwa wana taasisi imara, nidhamu ya kisiasa, na mfumo wa ulinzi wa kimkakati.

Leo hii, mtu anakuja kutoka nje, anafungua biashara nchini, anawachukua raia wenzake kutoka kwao kufanya kazi kuanzia ofisini mpaka usafi wa choo huku wananchi wa nchi husika wakishangilia kwa jina la wawekezaji na ‘uhuru wa biashara’.

Zipo nchi hata wauza pochi na vitumbua mtaani ni raia wa kigeni, ikiwa walibebwa na upepo wa ‘freedom of expression’ ndani ya Demokrasia.

Wengine wanakodisha mawakala wa kisiasa, wanapandikiza hoja kwenye mitandao, wanawachochea vijana kutukana Serikali kwa jina la uhuru wa kuongea. Wengine wanaeneza matusi, kejeli, na uzushi ili kuingilia mifumo ya ndani ya nchi kwa jina la demokrasia.

Wakati umefika ambapo tunapaswa kuwa na tafsiri mpya ya demokrasia kutokana na Mabadiliko ya kiutandawazi. Demokrasia isiyojengwa juu ya heshima, mipaka ya hoja, na ujenzi wa mshikamano na maelewano ni kelele tu.

Ni kweli kuwa uhuru wa kuongea unasaidia kushinikiza mabadiliko, lakini ni lazima tubainishe tofauti kati ya uhuru wa kusema na uhuru wa kudhalilisha. Tuwe na mfumo wa uhuru wenye maadili. Tuwe na sauti zenye dhamira, si hasira tu.

Watanzania wanapaswa kujua kwamba, Uhuru wa kuongea ni sawa na moto wa kupikia; ukitumiwa vibaya, unaweza kuunguza nyumba. Taifa lolote linalotaka kustawi lazima lijenge msingi wa mazungumzo yenye heshima, uhuru wa kueleza mawazo kwa hoja, na ujenzi wa taasisi zenye nguvu.

Zipo nchi leo zinaweza kuruhusu uhuru mpana hata wa matusi lakini kama hiyo ndio tafsiri ya demokrasia tunayotamani, basi tutakuwa tunajichimbia kaburi la heshima, uongozi, na uthabiti wa Kitaifa.

Demokrasia ya kweli hujengwa kwa hoja, si kwa makelele. Huimarishwa kwa taasisi, si kwa mitandao. Huwekwa kwenye msingi wa heshima, si matusi.

Demokrasia bila nidhamu ni kama upanga usio na ala unaweza kukukata wewe mwenyewe kabla hujamkata adui. Tujiulize. Je, bado tunataka kuwa na uhuru wa kuongea huku tukipoteza heshima yetu na tamaduni zetu? Tujibu kwa fikra si hisia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here