KATIKA kilele cha Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki, Banda la Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha lilipokea ugeni kutoka timu ya Council Health Management Team (CHMT) ikiongozwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri, Dkt. Wilford Kondo.
Katika banda hilo, wananchi walipata huduma mbalimbali za afya zikiwemo upimaji wa Virusi vya UKIMWI na Homa ya Ini.
Aidha, huduma ya lishe ilitolewa kwa wateja wote ambapo walipatiwa elimu kuhusu ulaji unaofaa ili kujikinga na magonjwa yatokanayo na lishe duni, pamoja na mbinu za matibabu hasa kwa watoto chini ya miaka mitano pale wanapobainika kuwa na changamoto za lishe.
Vilevile, huduma za uchunguzi na ushauri kuhusu magonjwa yasiyoambukizwa ziliendelea kutolewa, ikiwemo upimaji wa shinikizo la damu kwa lengo la kufahamu hali ya afya za wananchi na kuwashauri namna ya kuepuka maradhi yanayosababishwa na mtindo wa maisha usiofaa.