MSEMAJI wa kundi la watia nia wa nafasi ya ubunge na udiwani kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) maarufu kama G- 55, John Mrema amesema ndoto za wanachama wa chama hicho zaidi ya 200 zimezimwa kutokana na kiburi cha viongozi wa chama chao.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo, Aprili 22, 2025, Mrema alisema wanachama hao ni baadhi ya wale ambao tayari walionyesha nia ya kugombea kupitia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, lakini lipo kundi kubwa zaidi nyuma yao.
Alisema, kitendo cha viongozi wa Chadema kugoma kusaini Kanuni za maadili ya Uchaguzi, kumewaweka njiapanda watia nia hao ambao wana kiu ya kutaka kuwatumikia watanzania kwenye maeneo yao.
Mrema alisema, kitendo cha kutosaini kanuni za uchaguzi maana yake Chadema kimesusia uchaguzi na hakitashiriki tena hadi mwaka 2030 kama bado chama hicho kitaendelea kuwepo.
“Tumejifungia milango ya kushiriki uchaguzi, labda itokee miujiza,” alisema Mrema huku akiwashutumu viongozi wa Chadema kwa kutowaambia ukweli wanachama wao kuhusu hatma ya chama hicho kushiriki uchaguzi mkuu ujao.
Alisema, viongozi wanawaambia wanachama kwamba kuna fursa ya kusaini kanuni hizo, hivyo watapata sifa ya kushiriki uchaguzi jambo ambalo halina ukweli, kwani tayari wamepoteza nafasi hiyo na hawana njia nyingine ya kupinga maamuzi ya Tume ambayo imepewa mamlaka ya kuandaa kanuni na kuzisimamia.
“Tuliposhauri kuacha uamuzi wa kususia uchaguzi tulijua madhara yake, wameua ndoto za watu webgi nasasa wanajaribu kutafuta namna ya kurudi kwenye misingi,” alisema Mrema.
Aliendelea kusema, chama hicho ni cha mapambano na hakijawahi kususia wala kuogopa mapambano tangu kilipoanzishwa na alitaja chaguzi ambazo walishiriki licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi ukiwemo wa Kigoma Mjini, Tarime na Arumeru.
“Leo viongozi wetu wanasema tukishiriki uchaguzi tunapeleka watu wetu kufa, lakini wanasema tuzuie uchaguzi. Huu sio uchaguzi wa chama kimoja, tukienda kuzuia maana yake tunazuia wanachama wa vyama vingine ambao wanakwenda kutumia haki yao,” alisema na kuongeza, uamuzi huo unaweza kusababisha umwagaji wa damu.
Mrema alisema, bado ipo nafasi kwa viongozi wa Chadema na G-55 kujadiliana na kutafuta njia za kuepusha chama kusambaratika, na amewasihi wanachama wa chama hicho hususani watia nia kusubiri maelekezo ambayo watayatoa wakati wowote ili wapate mwongozo wa nini chakufanya na hatma ya ndoto zao.
“Watu wanaondoka kwenye chama. Wapo madiwani 85 wa Kata wanauliza wafanye nini? Watulie, kwasasa wakati tunaendelea kutafakaru na chana chetu, watia nia wasifanye maamuzi ya haraka wala wasikate tamaa, sio muda mrefu tutatoa njia bora ya kufanya ili tushikilie chama chama kisisambaratike,” alisema John Mrema.