CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemuonya Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Zanzibar, Omar Ali Shehe na kumtaka aache kutoa matamshi yenye vitisho.
Kadhalika CCM kimesema, dalili za matamshi ya vitisho ma mikwara ni kielelezo ACT kimeshashindwa vibaya uchaguzi Mkuu wa Oktoba Mwaka huu.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis, akiwa wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba alipokwenda kufuatilia zoezi la Uandikishaji wapiga kura.
Mbeto alisema, zoezi hilo lipo kwa mujibu wa sheria ya Uchaguzi Zanzibar, ambapo kila Mkaazi aliyeishi kwenye Jimbo moja kwa miezi 36, ndiye atakayekuwa mpiga kura halali si vinginevyo.
Alisema, madai kwamba kuna wananchi wa Pemba 60,000 (Elfu sitini) wenye vyeti vya kuzaliwa Zanzibar, lakini bado hawajaandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga kura, hayana mashiko.
“Mwambieni Omar Shehe aache vitisho vya kitoto na kutisha wenzake. Sisi ni wanaume wenzake hivyo asitutishe mchana kweupe. Anayemtisha yuko wapi hadi atishike kwa maneno yake?” alihoji Mbeto.
Akitoa ufafanuzi zaidi, Mbeto alisema kutokea hitilafu katika teknolojia ya mitandao ni mambo ya kawaida, hivyo hicho si kigezo kwa ACT kutaka kulazimisha watu ambao si wakaazi, waandikishe kwa lazima na shuruti.
“Sheria inawakataza watu ambao si Wakaazi wa Jimbo husika kuandikishwa kwenye Daftari la Wapiga Kura. Ikiwa si Mkaazi usiyetambuliwa na Sheha wako hawezi kuandikishwa na kuwa mpiga kura” alisisitiza Mbeto.
Alieleza, mtu anaweza kuwa na cheti cha kuzaliwa Zanzibar, lakini asiwe si sifa ya kuwa mpiga kura endapo tu hana sifa si Ukaazi wa jimbo husika au jina lake halijaorodheshwa kwenye Daftari la sheha wa shehia.
“ACT kukubali ukweli hakina ubavu wa kuishinda CCM wakati Rais Dkt. Hussein Mwinyi ndiye mgombea wa urais Zanzibar. Othman Masoud hana sifa hata kimoja ya kumshinda Rais Dkt. Mwinyi aliyeiletea Zanzibar mageuzi ya kimaendeleo,” alisisitiza Mwenezi huyo.
Hata hivyo, Mbeto aliwataka wananchi ambao ni Wakaazi wa Zanzibar kwa mujibu wa sheria ya Ukaazi inavyoelekeza, wajitokeze kwa wingi ili kutumia haki ya kuandikishwa na kuwa wapiga kura .
“ACT wanataka kuidanganya dunia na kupotosha ukweli. Zanzibar kuna sheria ya Ukaazi inayomtaka mwananchi ili awe mpiga kura lazima awe amekaa jimboni kwa miaka mitatu,” alieleza Mbeto.