Bunge lapitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira

0

BUNGE la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira wa Mwaka 2024, leo Februari 12, 2025 bungeni jijini Dodoma baada ya kufanyia marekebisho kadhaa kutoka katika mapendekezo ya Serikali.

Akiwasilisha maelezo ya muswada huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Yusuf Masauni amesema lengo la jumla la marekebisho yanayopendekezwa ni kuiwezesha Sheria hiyo kuendana na Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 na kutatua baadhi ya changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake.

Alisem, Ibara ya 3 ya Muswada inapendekeza marekebisho katika kifungu cha 13 ambacho kinapendekezwa kurekebishwa ili kujumuisha masuala yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi katika masuala ambayo yanasimamiwa na Waziri.

”Madhumuni ya mapendekezo ya marekebisho hayo ni kumpa Waziri mamlaka ya kudhibiti na kusimamia masuala ya mabadiliko ya tabianchi. Pia kuhakikisha kuwa Waziri mwenye dhamana na masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi anapata wasaa wa kutoa maoni yake kabla mipango ya kitaifa ya maendeleo haijapitishwa na mamlaka husika,” alisema Mhandisi Masauni.

Akiendelea, alisema Sehemu ya Tatu ya Sheria inapendekezewa kurekebishwa kwa kuongeza sehemu ndogo ya (e) inayoanzisha Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC), kubainisha malengo ya kuanzishwa Kituo na majukumu yake pamoja na kuweka masharti kuhusu uongozi na vyanzo vya fedha za Kituo.

Alisema, kituo hicho kilichopo mkoani Morogoro kimeendelea kutekeleza majukumu yake na kutokana na kutokutambuliwa kisheria kinashindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria ikiwemo kushindwa kuingia mikataba ya kitaifa na kimatifa na hivyo kukosa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na biashara ya kaboni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here