Na Mwandishi Wetu
BONDIA wa kike Conjestina Achieng ambaye amewahi kuipatia Kenya sifa kutokana na umahiri wake, amewataka watu wote ndani na nje ya nchi hiyo kupuuza taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba amefariki dunia.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Mombasa Women Empowerment Network, bondia huyo mweledi alisema anaendelea vyema na matibabu na kwamba anatazamia kurejea ulingoni hivi karibuni. “Ninaendelea vizuri. Napokea matibabu. Waliokuwa wakisema nimekufa nataka kuwaambia kuwa niko hai. Ni mbaya kusambaza habari za uwongo kuhusu mtu bila ukweli,”
Conjestina alisema, na kuwataka Wakenya kuendelea kumuombea. “Nataka kunyakua tena taji langu la IBF ndani ya nchi kabla sijastaafu. Ikiwa wafadhili wanaweza kujitokeza, nitafurahi na kuthamini,” alisema bondia huyo akiwa amejawa na furaha tele.