MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umepokea ugeni wa wajumbe wa Bodi ya Tume ya Mawasiliano ya Uganda (Uganda Communications Commission – UCC) waliofanya ziara ya mafunzo kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujifunza kuhusu utekelezaji wa miradi ya mawasiliano hasa maeneo ya vijijini nchini Tanzania.
Wajumbe hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya UCC, Dkt. Charity Baseball Mulenga, walifika katika ofisi za UCSAF jijini Dodoma ambapo walipokelewa na Menejimenti ya UCSAF wakiongozwa na Kaimu Mtendaji Mkuu, Mhandisi Albert Richard.

Katika ziara hiyo, UCSAF iliwasilisha mafanikio mbalimbali ya Mfuko katika kuhakikisha huduma za mawasiliano zinafika vijijini, ikiwemo ujenzi wa minara ya mawasiliano, usambazaji wa vifaa vya TEHAMA kwa shule za umma, pamoja na mipango ya baadaye ya kuhakikisha Watanzania wote wanafikishiwa huduma za mawasiliano.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa UCC, Dkt. Mulenga alipongeza jitihada za Serikali ya Tanzania kupitia UCSAF katika kukuza usawa wa mawasiliano, akibainisha kuwa wamejifunza mambo mengi muhimu watakayoweza kuyatumia katika kuboresha huduma za mawasiliano nchini Uganda.
Ugeni huu ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya mawasiliano, na kuchochea maendeleo endelevu kupitia teknolojia.
