Na Mwandishi Wetu, MAELEZO
MKUU wa Mkoa wa Kigoma, IGP (Mst) Balozi Simon Sirro amesema Serikali imetoa jumla ya Shilingi Bilioni 98 ili kuongeza upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya katika mkoa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma, Julai 19, 2025 kuelezea mafanikio ya Serikali yaliyopatikana katika mkoa huo kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema maboresho ya sekta ya afya yameongezeka idadi ya hospitali za Wilaya kutoka tatu (3) mwaka 2020 hadi nane (8) mwaka 2025 pia kuongezeka vituo vya afya kutoka 34 mwaka 2020 hadi 53.
Aidha, ameongeza kuwa idadi ya zahanati zinazotoa huduma katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo zimeongezeka kutoka 236 mwaka 2020 hadi 283 mwaka 2025 sanjari na ongezeko la nyumba za watumishi wa afya kutoka 384 mwaka 2020 hadi nyumba 416 mwaka 2025.
Katika hatua nyingine IGP (Mst) Balozi Simon Sirro aliema, Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa hospitali ya kanda ambayo itahusisha utoaji wa huduma za matibabu ya kibingwa ili kutoa fursa kwa wakazi wa ndani na nje ya mkoa huo na nchi jirani kupata huduma bora za matibabu na chunguzi za kiafya, sambamba na kuendelea ujenzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili Kampasi ya Kigoma ambao hadi sasa umefikia asilimia 14.