Na Veronica Simba – REA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko ameeleza kuwa vijiji vyote 108 vya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe vimekwishafikishiwa nishati ya umeme kupitia miradi inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Aidha, alisema kuwa katika Wilaya hiyo peke yake, Serikali imetumia Shilingi Bilioni 9.5 kupeleka umeme.
“Tunapeleka umeme katika vitongoji vyote vilivyobaki, ili watu wote wapate umeme,” aliongeza Dkt. Biteko wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ikwavila wilayani humo, mapema Februari 21, katika hafla ya kuwasha umeme katika Shule ya Msingi Ikwavila.
Naye Mbunge wa Wanging’ombe ambaye pia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Festo Dugange, amekiri na kuipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati na REA kwa kuvifikishia umeme vijiji vyote 108 vya Wilaya hiyo.
“Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, kati ya vitongoji 525 tulivyonavyo, watendaji wako wachapakazi tayari wametuletea umeme katika vitongoji 295,” alisema.
Akieleza zaidi, Dugange alisema katika Mwaka huu wa Fedha, Serikali imeanza utekelezaji wa miradi ya REA katika vitongoji vingine 72 huku vitongoji 158 vilivyobaki vikiwa na wakandarasi ambao wanaendelea na kazi.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Godfrey Chibulunje ameeleza kuwa, kwa sasa REA inatekeleza jumla ya miradi mitatu katika maeneo tofauti ya Wilaya ya Wanging’ombe.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili B pamoja na Mradi wa kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.
Kuhusu takwimu za Mkoa wa Njombe, ameeleza kuwa jumla ya vijiji 361 kati ya 381 vimekwishafikishiwa umeme wa REA, sawa na asilimia 94.75.
Aidha, vitongoji 1,148 kati ya 1,836 sawa na asilimia 62.5 tayari vimefikiwa na umeme kupitia miradi mbalimbali ya REA.
Viongozi wengine walioshiriki katika hafla hiyo ya kuwasha umeme ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Claudia Kitta na viongozi wengine wa Vyama vya Siasa na Serikali.