Na Naishooki Makeseni, MAELEZO
MKUU wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda, amesema jumla ya Shilingi Bilioni 85.8 zimetumika kuwezesha wananchi wa mkoa huo kiuchumi katika eneo la biashara na uwekezaji kupitia mikopo isiyo na riba inayotolewa kupitia halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye Ulemavu.
Mtanda amesema hayo Julai 16, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO Jijini Dodoma, kueleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika Mkoa wa Mwanza.
Alisema, katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu vilivyopewa mikopo ya asilimia 10 isiyo na riba vimeongezeka kutoka 630 hadi 1,856 pia kiwango cha mikopo iliyotolewa kimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 3.3 hadi Shilingi Bilioni 14.1.
Aidha, alisema kaya masikini zimeendelea kunufaika na mpango wa kuwezesha Kaya masikini – TASAF ambapo kaya 59,932 zimenufaika ambapo jumla ya Shilingi Bilioni 44 zimetolewa kwa walengwa kama ruzuku ya kuwasaidia kuboresha maisha yao ya kila siku.
Katika eneo la biashara na uwekezaji, Mtanda alisema idadi ya viwanda vikubwa imeongezeka kutoka 46 mwaka 2020 hadi viwanda 50 mwaka 2025 ambayo ni sawa na ongezeko la viwanda 4 huku idadi ya viwanda vya kati nayo ikiongezeka kutoka 109 mwaka 2020 hadi 116 mwaka 2025 na viwanda vidogo ikiongezeka kutoka 1,776 mwaka 2020 hadi viwanda 2,322 mwaka 2025 ambayo ni sawa na ongezeko la viwanda 546.
Kwa upande wa biashara zenye leseni Mtanda alisema imeongezeka kutoka 23,704 mwaka 2020 hadi 29,606 mwaka 2025 ambayo ni sawa na ongezeko la biashara zenye leseni 5,902.