Bilioni 51 za mradi wa TACTIC kuongeza thamani ya jiji la Mbeya

0

MRADI wa Uendelezaji Miji Tanzania (TACTIC) unatekeleza miradi yenye thamani ya Shilingi Bilioni 51 katika halmashauri ya jiji la Mbeya ikiwa ni uendelezaji wa jiji hilo katika eneo la miundombinu ya barabara, masoko na stendi.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa mradi wa TACTIC jiji la Mbeya, Mhandisi Yunus Nsegobya wakati akielezea hali ya utekelezaji wa mradi huo unaogharamiwa na mkopo nafuu toka Benki ya Dunia ambapo jiji la Mbeya ni miongoni mwa majiji yanayonufaika na mradi huo.

Ameeleza kuwa mradi wa TACTIC katika jiji la Mbeya unatekeleza ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa KM 12.3, taa za barabarani, mitaro ya maji ya mvua KM 6.41 na ujenzi wa jengo la ofisi la kusimamia mradi kwa gharama ya Shilingi Bilioni 21 ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 70.

Vile vile, ameongeza kuwa wanatekeleza miradi mingine ikiwemo ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi eneo la “Old Airport” na Soko Kuu eneo la “Sokomatola” kwa gharama ya Shilingi Bilioni 30 ambapo miradi hiyo ikikamilika itaongeza mapato ya halmashauri kutoka Bilioni 24 hadi kufikia Bilioni 35 hadi 40.

Aidha, ameishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio cha wananchi wa Mbeya kwa kuboresha miundombinu mbalimbali ambayo imepandisha thamani ya jiji hilo na wananchi sasa wananufaika na huduma za usafiri na usafirishaji, pia amewataka wananchi wa Mbeya kulinda miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

Naye, Mhandisi Boniface Kasambo Meneja wa TARURA wilaya ya Mbeya amesema miradi iliyotekelezwa ni ujenzi wa barabara ya Uyole-Itezi KM 1.8, Ilomba-Machinjioni KM 3.8, Kabwe-Block T KM 1.2, barabara ya Iziwa KM 2, barabara ya Kalobe KM 3.8 na mfereji wa maji ya mvua KM 6.41 ambapo barabara hizo zimeleta mabadiliko makubwa kwani sasa wakulima wanasafirisha mazao yao sokoni kwa urahisi.

Kwa upande wake, mkazi wa mtaa wa VETA-Machinjioni, Victor Mlay ameishukuru Serikali kwa miundombinu ya barabara ambayo imewezesha thamani ya maeneo yao kupanda, kuchochea biashara na kuboreka kwa huduma za usafiri na usafirishaji hivyo kuchangia kukua kwa fursa za kiuchumi na kijamii ambapo amesema taa za barabarani zikiwekwa mji utapendeza na biashara zitafanyika hadi usiku.

Mwalimu Ezekia Gwenino wa shule ya sekondari ya Uyole amesema hapo awali barabara zilikuwa na matope, mashimo, vumbi na maji yalikuwa yanajaa barabarani hali iliyopelekea kuwa na changamoto ya usafiri lakini sasahivi usafiri upo vizuri wanafunzi na walimu wanafika shuleni kwa wakati na amewaomba wananchi wenzake waitunze mifereji kwa kutotupa taka ili iweze kudumu muda mrefu.

Naye, Zena Nassor mfanyabiashara katika soko la Sokomatola ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa soko jipya na kubwa la Sokomatola ambalo likikamilika wateja wataongezeka na watafanya biashara zao vizuri katika mazingira mazuri.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here