Bilioni 30 kuongeza thamani ya jiji la Mbeya

0

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mohamed Mchengerwa amesema ujenzi wa Stendi Kuu ya Mabasi na Soko katika jiji la Mbeya vitakwenda kuongeza thamani ya Jiji hilo kwani itaboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Aliongeza, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha zaidi ya Shilingi Bilioni. 30 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu katika jiji la Mbeya.

Mchengerwa ameyasema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini Mikataba ya miradi ya ujenzi wa barabara, Kituo Kikuu cha Mabasi na Soko Kuu la Jiji hilo kupitia Mradi wa TACTIC iliyofanyika katika Viwanja vya Aiport ya zamani jijini Mbeya.

Alisema, ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi eneo la “Old Airport” na Soko Kuu eneo la “Sokomatola” utagharimu Jumla ya Shilingi Bilioni 30.12 na ni imani yetu sote pasina shaka kuwa miradi hii italeta mabadiliko chanya kwa wananchi wa Jiji la Mbeya na wageni mbalimbali ambao watanufaika huduma za usafiri na usafirishaji na ufanyaji wa biashara kwani nidhahiri kuwa thamani ya maeneo husika itapanda na hivyo kusababisha ongezeko la mapato kwenye Halmashauri.

Aidha, aliwataka wananchi wa Mbeya kulinda Miundombinu hiyo kwa kuwa inagharimu fedha nyingi na ni jukumu la wananchi kuitunza ili iweze kudumu kwa muda uliotarajiwa na kuhudumia vizazi vinavyokuja.

Naye Mbunge wa Mbeya Mjini ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, ameishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio cha Wananchi wa Mbeya kwa hatua ya kuanza kuboresha miundombinu mbalimbali katika Jiji la Mbeya ikiwemo barabara ambazo zimekuwa kero kwa miaka mingi.

Mikataba iliyosainiwa ni sehemu yamradi wa uboreshaji wa majiji, manispaa na miji ujulikanao kama Tanzania Cities Transforming Infrastructure and Competitiveness (TACTIC) inayotekelezwa kwa mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia utakaogharimu kiasi cha Dola za Kimarekami Milioni 410 na inatekelezwa katika miji 45 nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here