Benzema astaafu soka la Kimataifa

0

PARIS, Ufaransa

MSHAMBULIAJI Karim Benzema amestaafu kucheza soka ya kimataifa baada ya hapo awali kujiondoa kwenye kikosi cha Ufaransa kutokana na jeraha pajani alilopata siku moja kabla ya Kombe la Dunia kuanza nchini Qatar.

Baada ya kujumuishwa katika kikosi cha Didier Deschamps kilichoshiriki kwenye Kombe la Dunia, jeraha lilikatiza ndoto ya mshindi huyo wa tuzo ya Ballon d’Or 2022 ya Mchezaji Bora wa Dunia.

Kukosena kwa staa huyo wa klabu ya Real Madrid kulivuruga juhudi za Les Bleus kuhifadhi ubingwa, baada ya kuchapwa na Argentina fainali, Jumapili iliyopita.

Jina la nyota huyo aliyevumilia uhusiano mbaya dhidi ya Deschamps lilibakia kikosini, hata baada ya Ufaransa kufuzu kwa fainali, na wengi walimtarajia kurejea kikosini baada ya kuonekana akifanya mazoezi na klabu yake ya Madrid, lakini kocha Deschamps hakumuita.

Benzema alianza kuchezea Ufaransa kwa mara ya kwanza 2007 na kuwakilisha Taifa lake katika mashindano makubwa wakati wa Euro 2008 na 2012, pamoja na Kombe la Dunia la 2014.

Aliisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Nations League mwezi Oktoba 2021.

Benzema amestaafu baada ya kuchezea Ufaransa mara 97 na kufunga mabao 37, lakini sasa mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 35 atabakia kuitumikia klabu yake ya Real Madrid.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here