Bandari ya Tanga yaibeba Tanzania Kimataifa

0

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameelezea kuridhishwa na maboresho makubwa yaliyofanyika Bandari ya Tanga ikiwemo ujenzi wa gati mbili mpya.

Rais Samia alisema, Tanga sasa inajipambanua kama lango muhimu la biashara kwa Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla.

“Tulitamani kwa muda mrefu kuona meli kubwa zikitia nanga katika Bandari ya Tanga, shughuli za bandari zikishamiri, na vijana wengi wakipata ajira. Leo hii, hayo yote yamewezekana kwa uwekezaji wa Shilingi bilioni 429 uliofanywa katika maboresho ya bandari hii,” alisema Rais Samia.

Maboresho hayo yameongeza kina cha maji bandarini, kuwezesha meli kubwa kufunga moja kwa moja kwenye gati, tofauti na awali ambapo mizigo ilikuwa inashushwa baharini kisha kusafirishwa kwa matishari.

Maboresho hayo pia yamesaidia kupunguza muda wa kuhudumia meli kutoka siku kadhaa hadi siku mbili pekee.

Kwa sasa, Bandari ya Tanga imeongeza uwezo wake wa kuhudumia mizigo kutoka tani 400,000 mwaka 2019/2020 hadi tani 1,200,000 hivi sasa , ikiwa ni ongezeko la zaidi ya tani 700,000.

Mapato nayo yameongezeka mara mbili, kutoka Shilingi bilioni 17.27 hadi kufikia rekodi ya Shilingi bilioni 49 kwa miezi saba pekee ya mwaka huu wa fedha.

Rais Samia amebainisha kuwa, maboresho hayo yatanufaisha siyo tu wafanyabiashara bali pia serikali kupitia ongezeko la mapato na ukuaji wa sekta ya viwanda

“Natamani kurudisha hadhi ya Tanga – iwe Tanga ya viwanda, bandari kubwa na pia Tanga ya uvuvi. Hiki ndicho ninachokifanya,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ametangaza mpango wa kujenga barabara ya Handeni-Kiberashi-Kijungu-Singida (KM 340) kwa mfumo wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi (PPP).

Alisema, barabara hiyo itakuwa muhimu kwa usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Tanga kwenda maeneo mbalimbali nchini na Kimataifa. “

Tutaiwekea road tolls (tozo za barabara)ili mwekezaji anayejenga barabara hii aweze kurudisha gharama zake,” alisema.

Akihitimisha hotuba yake, Rais Samia amewataka wafanyakazi wa bandari kufanya kazi kwa ufanisi ili kushindana na bandari nyingine za Kimataifa, huku akihimiza matumizi ya teknolojia za kisasa.

“Tunashindana na bandari za mataifa mengine. Tukifanya kazi kwa bidii na kupunguza gharama za uendeshaji, Bandari ya Tanga itakuwa kitovu cha biashara Afrika Mashariki,” alihimiza.

Kwa maboresho hayo, Bandari ya Tanga imechukua nafasi yake kama lango muhimu kwa uchumi wa Tanzania, ikiwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa zaidi na kurahisisha biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine duniani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here