Bajeti ya TARURA Mkoa wa Mwanza yapanda kwa asilimia 300

0

KATIKA kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bajeti ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Mwanza imepanda kwa asilimia 300.

Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa TARURA Mkoa wa Mwanza Mhandisi Makori Kisari mbele ya Kamati ya Ukaguzi ya TARURA ilipofanya ziara ya Ukaguzi wa ujenzi wa miundombinu ya barabara mkoani humo hivi karibuni.

Mhandisi Makori ameileza Kamati hiyo kuwa bajeti ya TARURA mkoa wa Mwanza imepanda kutoka Shilingi Bilioni 8.4 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Shilingi Bilioni 25 mwaka 2024/2025.

Alisema, ongezeko hilo limewawezesha kuhudumia mtandao wa barabara wa mkoa huo wenye Wilaya saba na Halmashauri nane zaidi ya Kilomita 8000 kwa viwango tofauti ikiwemo lami, zege, mawe, changarawe na udongo.

“Ni suala la kuishukuru Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ilivyotuongezea bajeti hiyo na vyombo vyake vingine vinavyosimamia utekelezaji wa bajeti kuanzia Wizara ya TAMISEMI ambayo sisi tupo chini yake lakini pia na TARURA Makao Makuu,” alisema Mhandisi Makori.

Mhandisi Makori amefafanua kuwa mwaka jana wametekeza miradi yenye zaidi ya mikataba 79 na kuongeza kuwa wameshaanza mchakato wa manunuzi kwaajili ya mikataba ya mwaka 2025/2026 ili kuwahi kutekeleza miradi hiyo kabla kipindi cha mvua hakijaanza.

Kuhusu tatizo la msongamano wa magari katikati ya Jiji, Mhandisi Makori alisema mradi wa ujenzi wa barabara inayotoka Buhongwa mpaka Igoma yenye urefu wa KM 14 unaotekelezwa kupitia Mradi wa Uendelezaji Miji na Majiji Tanzania (TACTIC) una manufaa makubwa kwa Jiji la Mwanza.

Kwa mujibu wa Mhandisi Makori barabara hiyo itatumika kama barabara ya mchepuko kwa magari yote yanayotoka Mkoa wa Shinyanga na mikoa ya Simiyu na Mara kuingia jijini Mwanza kama hayahitaji kuingia katikati ya Jiji basi yanaweza kutumia barabara hiyo hiyo ili kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji bila sababu za msingi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi TARURA CPA. Ally Rashid alisema, wamekagua baadhi ya Miradi na lengo kubwa ni kujiridhisha kama Miradi inayotekelezwa inazingatia taratibu kwa mujibu wa mikataba waliyoingia.

Alisema, wanashukuru kwamba baadhi ya Miradi waliyoitembelea asilimia kubwa inafanya vizuri na kuongeza kuwa ipo baadhi imekamilika na mingine ipo katika hatua za mwisho za kukamilika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here