Baadhi ya mila na desturi zinakandamiza wanawake – Rais Samia

0

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inahitaji Sheria madhubuti kuhakikisha kuwa wanawake wanashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na umiliki wa rasilimali.

Rais Samia amesema hayo kwenye maadhimisho ya miaka 25 ya Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (Women in Law and Development in Africa – WiLDAF) yaliyofanyika ukumbi wa Serena.

Aidha, Rais Samia alisema licha ya takwimu kuonyesha kuwa asilimia kubwa ya wanawake wanajishughulisha na shughuli za uzalishaji, bado baadhi ya mila na desturi zinawafanya wanawake kuendelea kukandamizwa.

Rais Samia alisema, Sheria ni nyenzo kuu ya ufikiwaji wa usawa wa kijinsia na ustawi wa wanawake hivyo kutoa kipaumbele kwa wanawake ni jambo la lazima ili kuleta maendeleo.

Vile vile, Rais Samia alisema ipo haja ya kufanya tathmini ya Sheria zilizopo na kuona zina mchango gani kwa Watanzania na kuhakikisha kuwa zinakwenda ngazi za chini ili ziweze kutambuliwa na kufahamika kwa wananchi.

Kwa upande mwingine, Rais Samia alitoa wito kwa Sheria kutungwa na kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili kurahisisha kutoa elimu na ufahamu kwa wananchi.

Rais Samia ameiagiza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na Wasaidizi wa masuala ya Sheria kuwashirikisha wananchi na viongozi wa dini na kimila katika kuondoa vitendo vya udhalilishaji na ukandamizaji dhidi ya mwanamke.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here