📌 Askofu Mkuu Maimbo Mmdolwa ahimiza katiba ifuatwe
📌 Dkt. Biteko asema milango ya Serikali iko wazi kwa mazungumzo
📌 Asema Serikali inathamini mchango wa kanisa kwa jamii
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mhashamu Maimbo Mmdolwa amewahimiza Watanzania kushiriki katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025 na kuongeza kuwa nchi inaweza kuingia katika mgogoro mbaya wa kikatiba kama watasikiliza watu wanaotaka kuahirisha Uchaguzi Mkuu.
Askofu Mmdolwa amesema hayo Mei 11, 2025 jijini Mbeya katika ibada ya kuwekwa wakfu Canon Jacob William Kahemele kuwa Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini – Mbeya ambapo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi.
“Kwa kuwa Naibu Waziri Mkuu uko hapa na tuliombe Taifa zima kutoahirisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 kwa kuwa tutaingia katika mtanziko mkubwa na mgogoro wa kikatiba. Kama kuna changamoto zitafutiwe suluhu ziishe,”
Askofu Mmdolwa ameipongeza Serikali kwa ushirikiano wake na Taasisi za dini nchini na kuunga mkono Uhuru wa kuabudu ikiwa na lengo la kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Akizungumza mara baada ya ibada hiyo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema milango ya Serikali iko wazi chini ya uongozi wa wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwasihi wenye hoja kujongea kwa mazungumzo.
“Ninachoweza kusema kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu unakuwa uhuru na wa haki huku nchi ikiendelea kuwa na amani.
“Uchaguzi utafanyika kwa uhuru na haki kama katiba inavyotaka, waliposikika waliotaka marekebisho ya sheria Serikali ilipitia na kufanya marekebisho ya sheria zinazosimamia uchaguzi na leo milango ya Rais Mhe. Dkt. Samia ipo wazi kwa yeyote mwenye kutoa malalamiko yake ili nchi iende mbele,” alisema Dkt. Biteko.
Amewaasa Watanzania kuendelea kuiombea nchi ili amani iendelee kuwepo kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Dkt. Biteko alisema, Serikali inathamini mchango wa madhehebu yote ya dini, ikiwemo Kanisa la Anglikana. Katika nyanja za elimu, afya, maji, na maendeleo ya jamii, Serikali inashirikiana kwa karibu na taasisi za dini kwa lengo la kuimarisha huduma kwa wananchi.
Akitoa mfano wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini yenye makanisa 37 yanayosimamiwa na parish katika mikoa ya Songwe na Mbeya kupitia makanisa hayo yanasaidia kufikisha huduma ya kiroho kwa jamii.
“Kuanzia mwaka 2016 hadi 2025 Kanisa kwa kushirikiana na wadau limetumia zaidi ya shilingi bilioni tano kwa ajili ya kuendesha miradi ya “Dreams na Archive” kwa kusaidia Elimu Maalumu ya Vitendo ya kujikomboa Kiuchumi na Afya kwa Mabinti na Watoto wanaoishi na maambukizi ya UKIMWI katika maeneo ya Mbeya, Songwe na Tunduma,” alisema Dkt. Biteko.
Miradi hiyo imesaidia zaidi wananchi 160,000 waliokuwa na changamoto hizo za kijamii na kiuchumi. Aidha, imejiri zaidi ya watu 150 hivyo kuwaongezea kipato na kuwarahisishia maisha wananchi.
Pia, alisema Serikali itaendelea kushirikiana Kanisa la Anglikana kwa karibu zaidi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Vilevile, Dkt. Biteko amempongeza
Askofu Kahemela katika safari yake mpya ya kiutumishi huku akitoa wito kwa waumini wa Kanisa hilo kumtunza na kumsikiliza Askofu huyo pamoja na kumtia moyo kuwavumilia waumini wake endapo changamoto zitatokea.
“Tunakupongeza kwa moyo wa kujitoa kwa Mungu, kwa utii wako kwa wito wa kiutumishi, na kwa maono yako ya kiroho. Serikali inapenda kukupa uhakika kuwa tutaendelea kushirikiana kwa karibu na Dayosisi hii chini ya uongozi wako, kwa lengo la kukuza ustawi wa wananchi wetu, kulinda tunu zetu za taifa, na kuimarisha mshikamano wa kijamii na kitaifa,” alibainisha Dkt. Biteko.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kapteni mstaafu George Mkuchika amewaomba waumini wa kanisa la hilo kuwa na umoja na mshikano mara baada ya uchaguzi wa Askofu wa Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini na kutii viongozi wa dini ili kuendeleza kazi ya Mungu.
Aidha, alisema Serikali iliyopo ni sikivu na endapo kuna malalamiko yasikilizwe, na kuwa Uchaguzi usitenganishe Watanzania bali uwaaunganishe, pia amewataka watu wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali wafanye hivyo kwa kufuata utaratibu.
Awali, akihubiri katika ibada hiyo, Mhashamu Askofu Sospeter Ndenza alisema, Askofu ni Kuhani Mkuu na Mchungaji Mkuu kwa niaba ya Kristo na anasimamia nidhamu ya kanisa na kuona ibada zinasimamiwa na kufuata taratibu za kanisa pamoja na kusimamia utoaji wa huduma za sakrementi tofauti.
Alisema, wajibu huo ni mzito unahitaji uongozi na hekima ya Mungu.
“Jacob unahitaji kumuomba Mungu akupe hekima hasa katika dunia ya leo, leo unapokusidia kuwekwa wakfu unahitaji hekima na adili ili umwakilishe kristo,” alisema Mhashamu Askofu Ndenza.
Alisema, Askofu huyo asiogope vitisho kwa kuwa kutakuwa na watu watakao mpinga hata hivyo asitetereke badala yake ajue njia za Mungu na asitumie akili zake bali ajinyenyekeze kwa Mungu naye atamsaidia.
Naye Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini, Canon Jacob William Kahemele ameahidi kuwaombea viongozi wa Serikali ili waweze kuiongoza nchi kwa amani na utulivu.
“Wakati wa uongozi wetu tutahimiza sana watu kusali sana ili kukua kiroho kwa kuwa shetani mjanja sana na anadanganya watu kufuata njia za udanganyifu. Pia tutasisitiza sana uamsho wa kiroho ili watu wasiwe wachanga na kuyumbishwa huku na huko,” alisema Askofu Kahemele.
Alisema, wanaamini wameitwa kufanya majukumu makubwa kwa kutoa ibada, kutenda kazi kwa uaminifu sambamba na kusaidia wenye uhitaji.
Aidha, ametaja baadhi ya changamoto zinazowakumba vijana nchini za matumizi ya pombe kali, sigara na michezo ya kamari hivyo ameiomba Serikali kuzuia uholela wa uuzaji wa pombe kali na sigara.
Licha ya hayo ameipongeza Serikali kwa kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati mfano treni ya kisasa (SGR) na kuiomba kufikiria namna ya kuunganisha Mkoa wa Mbeya na Dar es salaam kwa kutumia treni hiyo ya kisasa ili kusaidia kukuza uchumi wa mkoa huo.
Ibada hiyo ya kumuweka wakfu Canon Jacob William Kahemele kuwa Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Dkt. Tulia Akson, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi.