RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewasisitiza mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali kuzingatia diplomasia ya uchumi na kuzitangaza fursa za uwekezaji ziliopo.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza na mabalozi wa Tanzania wa Nchi za Rwanda, Zimbabwe, Sweden na Msumbiji waliofika Ikulu kumuaga kabla ya kwenda katika vituo vyao vya kazi baada ya kuteuliwa hivi karibuni.
Amewahimiza mabalozi hao kufanya juhudi maalum za kuitangaza sera ya uchumi wa buluu na utalii katika mataifa hayo Ili kuvutia wawekezaji zaidi kuwekeza nchini.
Alisema, Zanzibar bado inahitaji wawekezaji wengi hususan katika sekta hizo kuu za kipaumbele kutokana na kuwepo kwa fursa nyingi ikiwemo uvuvi, utalii na mafuta na gesi.
Halikadhalika Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa suala la mahusiano ya kimataifa hivi sasa limeelekezwa zaidi katika uchumi hivyo wanapaswa kuzingatia zaidi kuimarisha uhusiano wa kiuchumi.
Ameyataja maeneo ambayo yana fursa za kutosha kuwa ni uwekezaji katika sekta ya bandari zikiwemo za makontena, usafirishaji wa mizigo na mafuta na gesi.
Akizungumzia sekta ya biashara amewaagiza mabalozi hao kuzitafutia masoko bidhaa za Tanzania ikiwa ni pamoja na viungo vinavyozalishwa kwa wingi hapa Zanzibar pamoja na utalii wa huduma na vivutio vya utalii ili kuwavutia watalii wa mataifa hayo kutembelea Zanzibar.
Nao Mabalozi hao wameahidi kuyatumia maelekezo ya Rais Dkt. Mwinyi kuwa ni nyenzo na dira ya kufanya Kazi zao kwa ufanisi pamoja na kuyazingatia maeneo muhimu ya kiuchumi kwa kushawishi uwekezaji.
Mabalozi walioaga nchi wanazoenda zikiwa kwenye mabano ni Balozi Dkt. Habibu Kambanga (Rwanda), Balozi CP Suzane Kaganda (Zimbabwe), Balozi Mobhare Matinyi (Sweden) na Balozi CP Hamad Hamad – (Msumbiji).