Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kuwa kitovu cha Utalii

0

Na Jacob Kasiri, Ruaha

MWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini – TANAPA Jen. Mst. George Waitara amesema Hifadhi ya Taifa Ruaha kuwa kitovu cha Utalii Kusini mwa Tanzania kutokana na ubora wa miundombinu ya kisasa ya utalii iliyowekezwa kupitia Mradi wa REGROW unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Aliyasema hayo Aprili 6, 2025 wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi sita inayotekelezwa katika hifadhi hiyo ya pili kwa ukubwa Tanzania ikiwa na ukubwa wa Kilometa za mraba 19,822 huku ikibeba mikoa ya Dodoma, Iringa huku eneo kubwa la hifadhi hiyo likiwa katika wilaya za Mbarali na Chunya zilizopo mkoani Mbeya.

Alisema, “Tumetembelea miradi sita (6), mitano imekamilika isipokuwa jengo la abiria la uwanja wa ndege Kiganga ambao ujenzi wake unaendelea, kwa hakika nimefurahishwa na usimamizi wa Menejimenti ya Ruaha kwa kuwa bega kwa bega na wakandarasi hao, kwa hifadhi ambazo bado miradi hii inasuasua itabidi tuwatume kwenu. Kwani ninyi mmekuwa mfano mzuri wa kuigwa na hifadhi nyingine.”

Hata hivyo, Waitara aliwataka Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Ruaha kuhakikisha inawasimamia Wakandarasi ili kukamilisha jengo la abiria lililofikia asilimia 92, likamilike ili lianze kutumika kwa ndege zitakazoshusha abiria (watalii) katika uwanja huo wenye uwezo wa kupokea ndege za uwezo wa kubeba abiria 50 kwa wakati mmoja.

Waitara aliongeza, “Kwa miradi mitano iliyokamilika ambayo ni Nyumba za kulala wageni (Cottages), Hostel, Kituo cha Ikolojia, Majengo kwa ajili ya malazi ya madereva na waongoza wageni pamoja na Kituo cha kutolea taarifa za uhifadhi na utalii ziwekewe thamani ili zianze kutumika, kwa kufanya hivyo tutavutia watalii wengi kutembelea hifadhi hii.”

Naye CPA. Hadija Ramadhani Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini – TANAPA na Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi na Utawala Bora alisema, “Kwa hakika Hifadhi ya Taifa Ruaha mmeitendea haki fedha ya REGROW, majengo yote yamependeza na ni mfano wa kuigwa kwa hakika kazi zingefanyika hivi kama taifa tungefika mbali hivyo niwahimize kuweka thamani ili majengo hayo yatumike kwani majengo yakikaa muda bila kutumika huharibika”.

Sambamba na ukamilishaji wa majengo hayo na miundombinu mingine ndani ya hifadhi hiyo inayotegemewa kuwa kitovu kikubwa cha utalii upande wa kusini mwa Tanzania, Wajumbe hao wa bodi walitaka kujua usimamizi wa masuala mbalimbali ya jengo hilo la abiria.

Akitoa ufafanuzi wa jinsi ya usimamizi wa jengo hilo Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara Massana Mwishawa alisema, “TANAPA tumejipanga kuhakikisha usalama, usafi na huduma mbalimbali zinatolewa na wataalamu wetu wa ndani kwani baadhi ya Maafisa na Askari wameshapewa mafunzo na wengine wataendelea kupewa mafunzo kuendana na mahitaji ya wakati huo.”

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Kanda ya Kusini – Godwell Meing’ataki alisema kuwa kukamilika kwa majengo hayo mapya yatayohudumia watalii na watu mbalimbali kumeongeza uhitaji wa watumishi, hivyo shirika wakati sasa shirika kuona namna bora ya kuongeza watumishi kwa ajili ya kutoa huduma bora kulingana na viwango vya kimataifa.

Kabla ya kuanza kwa ziara hiyo, Wajumbe hao wa Bodi pia walipata wasaa wa kusikiliza wasilisho kutoka kwa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Abel Mtui Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha kuhusu shughuli mbalimbali za Uhifadhi na utalii zinazotekelezwa huku matumizi ya teknolojia yakichukua nafasi kubwa katika uhifadhi na ukusanyaji wa maduhuli.

Hifadhi ya Taifa Ruaha imeendelea kuwa hazina kubwa nchini Tanzania kutokana na umuhimu wa kuhifadhi wanyama na ndege mbalimbali adimu na waliopo hatarini kutoweka pamoja na mto “The Great Ruaha” kama chanzo cha nishati katika mabwawa ya Mtera, Kidatu na Bwawa la Kimkakati la Mwl. Nyerere, maji kwa matumizi ya majumbani na uvuvi uliohalalishwa hususani bwawa la Mtera kwa ajili ya wananchi kujipatia kipato, hivyo kukauka kwake hakuiathiri hifadhi tu bali ni watanzania wengi wanaotegemea mto huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here