CCM: Jina la Sheikh Abeid Karume limebaki midomoni mwa Wazanzibari wazalendo

0

Na Mwandishi Maalum, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM ) kimesema kitaendelea kuenzi yale yote yaliyoanzishwa katika utawala wa Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Rais Hayati Mzee Abeid Amani Karume aliyeuwawa kikatili Aprili 7, mwaka 1972.

Pia, chama hicho bado kimeahidi kuwa kilichokufa ni kiwiliwili cha Mzee Karume lakini fikra, upeo, vitendo na maono yake yataendelezwa toka kizazi hadi kizazi.

Msimamo huo umetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamisi Mbeto Khamis, aliyesema kifo cha Mzee Karume miaka 53 iliyopita, kimeacha masikitiko na majonzi makubwa.

Mbeto alisema, CCM kinaamini kuwa kundi la Wapinga Mapinduzi Matukufu na maharamia wa madaraka ndio waliosuka njama za kukatisha maisha ya kiongozi huyo na kuuridisha nyuma maendeleo ya Zanzibar .

Alisema, kifo cha kiongozi huyo jasiri na shupavu, kitaendelea kukumbukwa na kila Mzanzibari kutokana na uwezo, upeo na maono ya mbali aliojaliwa kuwa nayo kiongozi huyo mzalendo.

“CCM inaahidi kuendelea kuenzi fikra, Sera na mikakati iliotumika katika Awamu ya kwanza yaliowaletea wananchi maendeleo chini ya ASP. Tuna jukumu la kuendeleza na kusimamia mema yote kutekelezwa na kuendelezwa,” alisisitiza.

Aidha, aliwahimiza wananchi wa Zanzibar kutoacha kumuombea dua kwa mungu Kiongozi huyo azidi kumpa makaazi mema huko aliko na kumsamehe makosa yake yote.

“Alikuwa kiongozi shujaa na shupavu aliyewaunganisha Wazanzibari tokea enzi za African Association Mwaka 1935 hadi kilipoundwa ASP mwaka 1957. Lakini pia ndiye Jemedari Mkuu wa Mapinduzi Zanzibar Januari Mwaka 1964,” alieleza.

Katibu huyo Mwenezi alisema, mema yaliyofanywa na Serikali ya Mzee Karume katika uongozi wake wa miaka nane, yatazidi kukumbukwa na wananachi wa Zanzibar, pia kwa kuanzisha mchakato uliounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania April 26 mwaka 1964 miaka 61 iliyopita.

“Hatuwezi kuzungumzia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kusahau sera na juhudi za vyama vya ASP na TANU. Uamuzi wa waasisi wawili wa Mataifa yetu Hayati Sheikh Abeid Karume na mwenzake Marehemu Mwalimu Julius Nyerere utaendelea kuenziwa,” alisema Katibu huyo Mwenezi.

Kadhalika aliongeza kusema, pamoja na miaka 53 kupita tokea Kiongozi huyo alipouawa na genge la wapinga Mapinduzi, jina lake halijatoka midomoni mwa Wazanzibari Wazalendo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here