Mbeto: CCM kinajiandaa kioganaizesheni kushiriki Uchaguzi Mkuu Oktoba

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinaendelea na maandalizi ya kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba Mwaka huu kama Katiba na Sheria zinavyoelekeza kila baada ya miaka mitano kutafanyika Uchaguzi Mkuu.

Pia, CCM kimewataka watanzania kupuuza maneno ya baadhi ya viongozi wa vyama vinavyodai vitazuia Uchaguzi Mkuu mwaka huu usifanyike kwa utashi wao.

Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis aliyesema kalenda ya Uchaguzi Mkuu iko vile vile kwa mujibu wa Katiba na sheria.

Mbeto alisema, Uchaguzi si shuruti ya mtu, hiari ya kiongozi fulani au chama cha siasa, bali kinakachoelekeza uchaguzi kufanyika au kutofanyika ni matakwa ya Katiba na sheria.

Alisema, zipo sababu kadhaa zilizotajwa katika katiba na kufanya uchaguzi aidha uahairishwe au usogezwe mbele, lakini si kutokana na utashi binafsi wa mtu au chama chake.

“Uchaguzi wa nchi yoyote hauwezi kuzuiwa kwa shinikizo aidha la kisiasa au kwa shuruti toka Jumuiya fulani. Mtu anapokuwa na fikra hizo ni kama kuota ndoto alizowahi kuota Abunuwasi katika zama za kale,” alisema Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi amewataka wanachama na viongozi wa CCM katika ngazi mbalimbali za chama, kuendelea na mikakati ya maandalizi ya kishiriki uchaguzi mkuu kwa kuwa uchaguzi ni mchakato wa maandalizi ya mapema.

“Msikubali kuvisikiliza vyama vinavyodai havitashiriki uchaguzi. Viongozi wao hawana muamana. Ni waongo wanaoweza kugeuza maneno yao muda wowote. Huenda wanasema hivyo kwa lengo la kuifanya CCM ipweteke na kujisahau,” alieleza.

Mbeto alisema, kwa mujibu we Katiba ya mwaka 1977, sheria zake na muundo wa Tume ya Uchguzi wa sasa, upinzani umeshawahi kupata viti vya Madiwani, Wabunge, Wawakilishi ikiwemo kura za urais

Aidha, Mbeto alisema upinzani baada ya kuona miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita umefanya kazi kubwa ya utekelezaji wa Ilani na kuleta maendeleo ya aina yake, imeanza kuhofia na kubaini kupata majimbo na viti vichache.

“Tunajua kuwa upinzani umeshangazwa na kasi ya maendeleo yanayoonekana nchini kutokana na kasi ya kiutendaji wa kisera iliyofanyika. Hofu yao si Tume ya Uchaguzi wala sheria bali hawana cha kuwaeleza wananchi ili wapigiwe kura,” alisisitiza Mbeto.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here