Sekta ya maji kuendelea kusaidia wahitaji katika jamii

0

WIZARA ya Maji pamoja na Taasisi zake imechangia gharama za matibabu ya Watoto wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo ili kuwezesha kupata matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa tukio la kukabidhi mfano wa hundi ya mchango huo, Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri alisema kwamba, suala la Afya ni suala mtambuka ambalo linapaswa kubebwa na Sekta zote muhimu, hivyo ni wajibu wa Jamii kuendelea kurudisha tabasamu kwa kuchangia watoto wanaopitia changamoto za magonjwa mbalimbali ikiwepo magonjwa ya moyo.

“Tunatambua kuwa afya ndio msingi mkubwa wa kwanza kwenye maisha, hivyo mwaka huu tumeamua kusherehekea Wiki ya Maji kwa kuwagusa watoto wenye changamoto ya moyo ili kurudisha tabasamu la uhai wao tena. Ndio maana leo tumechangia kiasi cha Shilingi Milioni 20 kama matibabu kwa watoto watano walio na changamoto za Afya,” alisema Mhandisi Waziri.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Dkt. Tulizo Shemu ameishukuru Wizara ya Maji kwa kugusa maisha ya wagonjwa hao kwani uhitaji ni mkubwa na sehemu Wizara ilipochangia imesaidia kupunguza hatua kubwa.

“Kwa kawaida gharama za matibabu haya ni huanzia milioni nne kwa mgonjwa mmoja, ambapo kwa hali zetu za kitanzania ni ngumu sana mzazi au mlezi kumudu gharama hizi,” alisema Dkt. Msheri.

Nae Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Everlasting Lyaro alisema, Mamlaka imeanza mashirikiano na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kama sehemu ya kurudisha kwa jamii kupitia huduma inayozitoa na pia kurejesha tabasamu kwa Watoto na walezi wanaopitia changamoto za magonjwa ya moyo hapa Nchini.

“DAWASA na JKCI ni ndugu, tunafanya kazi pamoja, hivi karibuni tulishirikiana katika zoezi la kupima afya kwa Watumishi 300 wa DAWASA katika maandalizi ya kupanda Mlima Kilimanjaro, na sasa tumekuja kuchangia matibabu kwa Watoto wenye changamoto ya moyo, tunaandaa mpango endelevu kwa ajili ya mashirikiano haya na awamu ijayo tutafanya zaidi ya hapa”. alisema Lyaro.

Maadhimisho ya Wiki ya Maji Kitaifa hufanyika tarehe 16 hadi 22 Machi kila mwaka ambapo kwa mwaka huu 2025 Kauli mbiu ni “Uhifadhi wa Uoto wa asili kwa uhakika wa Maji

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here