KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeeleza kuridhishwa na utendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) katika Bandari ya Tanga, hasa baada ya maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali bandarini hapo.
Akizungumza baada ya ziara ya Kamati hiyo kukagua miradi ya maboresho ya sekta ya uchukuzi mkoani Tanga, Mwenyekiti wa Kamati, Moshi Kakoso, ametoa pongezi kwa Serikali na TPA kwa juhudi kubwa zilizofanikisha ongezeko la ufanisi na mapato bandarini.
“Tunatoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais, Wizara ya Uchukuzi na TPA kwa maboresho makubwa yaliyofanyika katika Bandari ya Tanga. Bandari sasa ufanisi unaonekana na mapato yameongezeka, hakika tumeridhishwa,” alisema Kakoso.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ameishukuru Kamati hiyo kwa kutembelea na kujionea kazi kubwa inayofanywa na serikali katika sekta ya uchukuzi, huku akiahidi kuwa maoni na ushauri waliotoa yatafanyiwa kazi ili kuendelea kuifungua Tanga kiuchumi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, alisema kukamilika kwa awamu mbili za maboresho ya Bandari ya Tanga kwa gharama ya Shilingi Bilioni 429.1 kumekuwa chachu ya maendeleo na ufunguo kwa ushoroba wa Kaskazini.
“Manufaa mtambuka ya Bandari ya Tanga yatapelekea maeneo yanayozunguka bandari kufunguka kiuchumi, hivyo ushirikiano na wadau wote, ikiwemo Kamati ya Bunge, ni muhimu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa,” alisema Mbossa.
Mbossa ameongeza kuwa, TPA itaendelea kushirikiana na Serikali, Bunge na wadau wa sekta ya bandari ili kuhakikisha miundombinu inaboreshwa zaidi na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.