‘Rais Samia ametoa kipaumbele kwa Serikali za mitaa kuchochea maendeleo’

0

OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuweka mkazo katika kuimarisha serikali za mitaa kama chachu ya maendeleo ya wananchi kwa kuongeza rasilimali, kuboresha mifumo ya utendaji, na kuimarisha uwajibikaji wa viongozi wa halmashauri.

Waziri Mchengerwa amesema hayo Machi 11, 2025 kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika jijini Dodoma.

“Maendeleo siyo ahadi, bali ni hatua zinazochukuliwa kila siku kwa vitendo. Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha serikali za mitaa zinakuwa msingi wa maendeleo ya wananchi.”

“Serikali yake imeonesha kuwa maendeleo yanaanzia chini kwenda juu, na kwa kuimarisha serikali za mitaa, tumewawezesha wananchi kushiriki moja kwa moja katika mchakato wa maendeleo,” alisema Mchengerwa.

Ameeleza kuwa, uwekezaji mkubwa umefanyika katika sekta ya elimu, afya, na miundombinu, hatua inayowezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

Aidha, Waziri Mchengerwa amewahimiza viongozi wa Serikali za mitaa kuwa wabunifu, kuzingatia uadilifu katika utendaji wao, na kushirikiana na serikali kuu ili kuhakikisha maendeleo ya taifa yanapiga hatua kwa kasi zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here