ACT Wazalendo inakufa Z’bar kwa kukosa hoja, Chadema kifo cha asili

0

Mwandishi Wetu

NI mwaka wa Uchaguzi Mkuu, vyama vya siasa vinatakiwa kujipanga kwa kuandaa, dira na sera ambazo wataziwasilisha kwa wananchi ili waweze kupata uungwaji mkono.

Mwishoni mwa mwaka jana 2024, tumeshuhudia uchaguzi wa Serikali za mitaa na matokeo wengi wanayafahamu; CCM ilishinda kwa kishindo.

Mwezi Machi unakatika, tunakaribia kwenda April, kwa maana tumebakiwa na miezi sita kabla ya kuingia katika Uchaguzi Mkuu 2025.

CCM wanazidi kujipanga, baada ya kishindo cha Serikali za mitaa ambako ndipo walipo wapiga kura, mikutano baina ya viongozi wa juu wa chama na wale wa ngazi ya chini inaendelea.

Vyama vikuu vya upinzani bado vipo njia panda, Chadema wapo kwenye ‘No Reform No Election’, wakimaanisha bila mabadiliko hakuna uchaguzi, zigo lote wakiwatupia wanachama wao wachache waliobakia.

Wanasema nguvu ya umma ndio itaamua iwapo uchaguzi utafanyika au la; wakimaanisha marekebisho ya Katiba, lakini mbaya zaidi hao wanachama wao hawajui viongozi wao wanataka nini na hata marekebisho ya Katiba yaliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka jana 2024 hawayajui.

Kwamba, marekebisho ya Katiba yakoje na yanasema nini, wanachama hawajaambiwi, lakini wanatangazwa kuwa wao ndio watakaoamua hatma ya uchaguzi wa mwaka huu.

Wenzao ACT Wazalendo wanatafuta washirika wa kuungana nao kwenye Uchaguzi Mkuu ama kwa kuungana mkono au kusaidizana baadhi ya mambo angalau viti vichache vya ubunge na udiwani vipatikane.

Viti hivyo vikipatikana maana yake ruzuku kwenye chama itaongezeka na viongozi watakata pesa walizotumia kwenye shughuli za chama na kulipana posho za vikao.

Makamu Mwenyekiti ACT Wazalendo Zanzibar, Jussa Ismail Ladhu na mwenzake wa Bara, Ado Shaibu wamezunguka ofisi za vyama vyote vya siasa vilivyokuwa na ushawishi siku za nyuma lakini bado mambo magumu.

Wamefanya hivyo angalau kupata uungwaji mkono Bara maana Zanzibar wameshapoteza mwelekeo kwani kero nyingi zimetatuliwa na nyongeza juu.

Tumaini halipo kwenye Ubunge wala Uwakilishi Pemba wala Unguja achilia mbali suala la Urais wa Zanzibar.

Hali hiyo kulingana na duru za kisiasa visiwani humo, ndio maana wakaona bora wajaribu Bara kwa kuunganisha nguvu na wengine maana pekee yao hawawezi.

Hawawezi kutokana na ukweli kuwa ahadi za CCM kwa Wazanzibari zote zimetimizwa na kupitiliza chini ya Rais wa sasa Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Ametimiza ahadi zote kwa wananchi na chache zilizobaki ameahidi mwenyewe kuwa kabla ya Oktoba zitakuwa zimekamilika katika kauli mbiu ya uchumi wa bluu na mabadiliko ya kiuchumi Zanzibar.

Ahadi ambazo bado na ameahidi kuzitekeleza kabla ya Oktoba Mwaka huu 2025 ni pamoja na zile ambazo aliziahidi katikati ya kipindi chake cha uongozi, lakini zilizo katika Ilani ya chama hicho, wenyewe wanasema hadaiwi.

Wabunge na wawakilishi wa ACT Wazalendo hawana hoja kwa wapiga kura, walisema tuchagueni ACT tuwajengee barabara, tayari zimejengwa, nitaleta maji, yapo.

Chadema wamekataa ushirika na ACT Wazalendo kulingana na habari za ndani ya chama hicho wakiamini kuwa wao ni chama kikubwa akihitajI makando kando ya chama kingine

NCCR-Mageuzi wakawakuta nao hawajielewi, wapo kama hawapo na duru zaidi za kisiasa ndani zinaeleza kuwa vyama vingi hali si shwari wananchi walisha vichoka kitambo.bWanaona ni kama NGO’s za viongozi ambao wapo kwa ajili ya maslahi yao.

Baadhi ya viongozi wao waandamizi Chadema wapo Ulaya na Marekani akiwemo Mwenyekiti wa zamani aliyeng’olewa kwenye nafasi yake hiyo, Freeman Mbowe.

Wiki iliyopita kukabandikwa tangazo katika mitandao ya jamii likimuhusisha aliyekuwa mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi akisema anagombea tena jimboni humo.

Sugu siku chache baadae kalikana tangazo kupitia akaunti yake ya X zamani Tweeter akisema “Sijatangaza popote, nipo zangu busy naongea viingereza tu hapa USA! NB: Huu ni ….. kama … mwingine tu wa machawa.”

Uchaguzi Mkuu ndani ya chama hicho uliomuweka madarakani Mwenyekiti mpya Tundu Lissu unatajwa kukisambaratisha chama.

Chama hicho hadi hivi sasa kina vugu vugu la mgogoro ambao unatokana na baadhi ya wanachama kuona wanataka kudhulumiwa haki yao ya Kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa.

Wengine chama kimewakatisha tamaa na ndio maana wakaona bora kukimbilia ughaibuni na mbaya zaidi wanachama hawaambiwi ukweli.

Nguvu ya chama ni wanachama na kutokana na mwenendo ulivyo ni wazi kuwa kifo cha kisiasa cha Chadema na ACT Wazalendo havipo mbali na pengine kimojawapo kinaweza kubaki kwa msajili wa vyama vya siasa, lakini sio kiutendaji kwa umma, tujipe muda.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here