CCM: ACT ikimsimamisha Othman ushindi bila jasho Zbar

0

Na Mwandishi Maalum, Zanzibar

CHAMA Cha Mapinduzi kimeihakikishia dunia kuwa ikiwa ACT Wazalendo watamsimamisha Mwenyekiti wake, Masoud Othman Masoud, kwenye nafasi ya urais Z’bar, CCM kitashinda bila kutoka jasho jingi.

Kimewaahidi Wazanzibari ifikapo Oktoba mwaka huu, CCM kitashinda kwa zaidi ya kura asilimia 80.2 kuliko wakati wowote katika historia ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar.

Ahadi hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar Idara ya Itikadi , Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamisi, kufuatia matamshi ya Othman aliyedai zama ya CCM kiutawala Zanzibar itafikia ukomo mwaka huu.

Othman ndiye Makamo wa kwanza wa Rais chini ya Serikali ya umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) toka chama cha ACT Wazalendo.

Alisema, kama kweli ACT Wazalendo kitamsimamisha Othman na kudhani atamshinda Rais wa Zanzibar Dkt. Huseein Ali Mwinyi ambaye amefanya mageuzi makubwa ya kimaendeleo, CCM kitashinda mapema kabla ya saa 5 asubuhi.

“Tusiandikie mate ilhali wino ungalipo. Hayati Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alikuwa gwiji wa siasa na tambo hakukiweza CCM. Alishindwa toka 1995 hadi 2020, hivyo kwa sasa ACT hakina mgombea mwenye ubavu wa kuitingisha CCM,” alisema Mbeto.

Aidha, Katibu huyo Mwenezi ameshangazwa na matamshi yaliyotamkwa na Waziri wa Afya SMZ, Nassor Ahmed Mazrui, aliyedai Zanzibar inakabiliwa na maisha magumu huku na kwamba kuna watu hupata maradhi kwa kukosa shibe.

“Mazrui ni Waziri toka ACT aliyewahi kusifu hadharani maendeleo yaliyoletwa na Serikali ya Rais Dkt. Mwinyi. Itawashangaza wananchi kumsikia Mazrui akitoa maneno ya kubeza maendeleo. Hapo ndipo itakapodhihirisha viongozi wa ACT wamebobea kwa unafiki wa kisiasa,” alisema.

Hata hivyo, Mbeto alisema vyovyote itakavyokuwa madai ya kusema Zanzibar haijapiga hatua za maendeleo wakati huduma za jamii zikiimarika , wananchi hawatakubali kufungwa vitambaa machoni mwao iwe hawaoni yaliyofanywa na Serikali.

“Viongozi wa ACT punguzeni uongo acheni wananchi wenyewe waseme. Wana macho yanayoona kila kitu kilichofanyika. Nyinyi mnapochukua jukumu la kuwasemea na kuwavunjia heshima. Wananchi wataendelea kuwadharau kwa kuwaongopea wakati wanaona,” alieleza Mbeto.

Katibu huyo Mwenezi alisema, kama ni mabadiliko ya maendeleo, wananchi wanashuhudia yaliyofanyika katika sekta za afya, elimu, utalii, miundombinu, ajira, ujenzi wa vituo vya afya, hospitali, masoko na barabara Unguja na Pemba.

“Othman na wenzako acheni siasa za uongo na kuwafanya wananchi hawajitambui. Yaliyofanywa na Serikali ya Rais Dkt. Mwinyi yanaonekana. Hakuna mwananachi atakayewamini viongozi waongo wakati kila kilichofanywa na SMZ kinaoonekana,” alisisitiza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here