MKURUGENZI wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Msajili wa Hazina, Amos Nnko amefariki dunia.
Nnko amefariki kwenye ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Same, mkoani Kilimanjaro, Jumapili, Disemba 22, 2024.
Hayo yamethibitishwa na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu leo Jumatatu, Disemba 23, 2024 kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari
Aidha, mbali na kifo cha Mkurugenzi huyo, mtoto wake wa kwanza Maureen Nnko naye amepoteza maisha.
Taarifa hiyo imeelezwa kuwa, mke wa marehemu, Agnes Nnko na watoto; Marilyn, Melvin pamoja na mwanafamilia mwingine, Sylvana wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya KCMC na Mawenzi.
Mchechu alimuelezea marehemu Nnko kama mchapakazi, muadilifu na mtu wa watu.
“Tumepokea taarifa za kifo cha Nnko kwa masikitiko makubwa sana. Tumepoteza nguzo muhimu,” alisema Mchechu.
Sanjari na hilo, alitoa pole kwa familia ya marehemu huku akiwaombea majeruhi wa ajali hiyo uponyaji wa haraka.
Mchechu alisema, taratibu za mazishi zinaendelea kuratibiwa huko Tengeru, Arusha kwa ushirikiano wa familia ya marehemu na Ofisi ya Msajili wa Hazina.