BENKI ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) kupitia Mradi wa kupunguza athari za UVIKO 19 “Emergency and Recovery Support for Biodiversity Tanzania (ERB)” ambao upo chini ya Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS), umekabidhi magari matano na mitambo miwili kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo iliyofanyika leo Disemba 2, 2024, kwenye ukumbi wa Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS), jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana alisema, vina thamani takribani Shilingi Bilioni 6.4 za Kitanzania.
Alisema, vifaa hivyo vilivyokabidhiwa leo, ni sehemu ya magari (maroli) nane na mitambo mitano ambayo imetolewa kwa ajili ya kusaidia shughuli za uhifadhi, utalii na kijamii, ambapo vitatumika kwenye hifadhi ya Serengeti, hifadhi ya Taifa ya Nyerere na Pori la akiba la Selou.
Dkt. Chana alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Ujerumani ambayo kwenye hafla hiyo iliwakilishwa na Julia Kroberg kwa niaba ya Balozi, benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) iliyowakilishwa na Jennifer Woelf na Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS), kwa kuwezesha shughuli za uhifadhi nchini.
Aidha, alitoa maagizo kwa Bodi, wakuu wa TANAPA na TAWA kuhakikisha vifaa na mitambo hiyo inatumika kwa kazi zilizokusudiwa na inatunzwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za matumizi ya vifaa vya Serikali.
Alisema, mitambo waliyokabidhiwa itatumika kwa ajili ya kuchimbia visima, kujengea Barabara na shughuli nyingine za kijamii na hifadhi ambazo watapewa vifaa hivyo.
“Tumepokea, tumepewa dhamana kwa niaba ya watanzania Milioni 62, nawahakikishia vifaa hivi na miradi mingine itasimamiwa kwa umakini,” alisema Waziri Chana.
Katika hatua nyingine, Waziri Dkt. Pindi Chana alisema, Serikali kupitia mradi wa ERB, itaendelea kununua vifaa mbalimbali kwa ajili ya kulinda uhai wa watanzania waliopo Jirani na hifadhi, sambamba na shughuli mbalimbali za uhifadhi yakiwemo matrekta, mabasi, magari, ndege na boti.