Dkt.Mpango apongeza ubunifu wa hati fungani ya Miundombinu

0

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amezindua hati fungani ya Miundombinu iliyopewa jina la ‘Samia Infrastructure Bond,’ maalum kwa ajili ya kuwawezesha wakandarasi wazawa wanao husika na ujenzi wa barabara za vijijini na mijini zinazo simamiwa na Wakala wa barabara za vijijini na mijini -TARURA.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesisitiza ubunifu kwa TARURA na kuwaasa kutumia uwepo wa fursa za fedha za mikopo nafuu na ruzuku zinazotolewa na mashirika na taasisi mbalimbali duniani katika kukabiliana na changamoto ya fedha inayowakabili baadhi ya wakandarasi wazawa.

Katika kutambua mchango wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI Dkt. Mpango amewatunuku vyeti watendaji wa juu wa idara na sekta mbalimbali zilizo chini ya ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI ikiwa ni kutambua utendaji kazi wao unaozingatia ubunifu katika utatuzi wa changamoto mbalimbali hasa za miundo mbinu ya barabara.

Miongoni mwa watendaji waliotunukiwa vyeti vya shukrani kwa ubunifu na utendaji kazi wao uliotukuka ni Pamoja na katibu Mkuu OR – TAMISEMI Adolf Ndunguru, Naibu katibu Mkuu Miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila, Mkurugenzi wa Miundombinu OR – TAMISEMI Mhandisi Gilbert Moga, CPA Jacobo Nyauringo, na Mtendaji mkuu wa Wakala wa barabara za vijijini na mijini TARURA Mhandisi Victor Seif.

Awali, Waziri wa Nchi OR – TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa alisema ‘Samia Infrastructure Bond’ ni maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na ishara ya dhamira yake ya kuleta mabadiliko ya kweli katika sekta ya miundombinu na uchumi wa Taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here