WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema, matumizi ya mfumo wa Kielektroniki wa Baraza la Mawaziri utasaidia kuboresha utendaji kazi na kuleta ufanisi zaidi katika kuwahudumia wananchi.
Alisema, maboresho hayo ya matumizi ya mfumo wa Kielektroniki yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matumizi ya karatasi katika vikao vya Serikali, hususan Baraza la Mawaziri, hivyo kupunguza changamoto ikiwemo kuchelewa kwa taarifa, gharama kubwa za uchapaji na hatari ya upotevu wa taarifa muhimu.
Alisema hayo leo (Jumatatu, Novemba 11, 2024) wakati akifunga Mkutano wa Kazi wa Mawaziri na Naibu Mawaziri kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza La Mawaziri (e-CABINET), kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Aliongeza, hatua hiyo inatokana na jitihada na malengo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kusisitiza umuhimu wa Mawaziri na watumishi wa umma kuzingatia mabadiliko ya kiteknolojia katika utendaji kazi,
“Matokeo ya mwaka 2023 ya ulinganifu baina ya nchi katika muktadha wa Ukomavu wa Matumizi ya Teknolojia Serikalini (Government Technical Maturity Index), nchi yetu ilishika nafasi ya tatu (3) ikilinganishwa na nchi nyingine Barani Afrika. “Tunampongeza na kumtakia kila la kheri Rais Dkt. Samia aendelee kubuni zaidi kwa manufaa ya Taifa letu . ”
Kadhalika, Waziri Mkuu alisema, mkutano huo kuhusu matumizi ya mfumo wa Kielektroniki wa Baraza la Mawaziri ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuhakikisha kwamba Mawaziri na watumishi wa umma wanakuwa na ujuzi wa kisasa wa uendeshaji wa shughuli za Serikali na utumishi kwa ujumla.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu alisema, uanzishwaji wa mfumo huo wa Kielektroniki wa Baraza la Mawaziri ni utekelezaji wa Ibara za 102 na 103 za Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 zinazoelekeza Serikali kuhakikisha kuwa sayansi, teknolojia na ubunifu vinatumika kikamilifu katika kuendesha sekta za kukuza uchumi kwa lengo la kufikia uchumi wa hadhi ya kipato cha kati ambao ni shindani, jumuishi na unaoongozwa na viwanda.
Kwa Upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amewapongeza wataalam kutoka Wakala wa Serikali Mtandao kwa kufanikisha mafunzo hayo. “Tunaamini tumeelewa kwa kiwango kikubwa sana. ”
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alisema, mafunzo hayo ni mwendelezo wa mpango wa Serikali kwenda kwenye matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza La Mawaziri (e-CABINET) mchakato ambao ulikuwa wa muda mrefu kupitia wataalam wa Wakala wa Serikali Mtandao.