Na Mwandishi Wetu
HOFU ya kutapeliwa imetanda kwa mamia ya watanzania waliowekeza fedha zao kwenye mradi wa ufugaji nguruwe unaosimamiwa na Kampuni ya Pigs Invest International PLC ambayo inaendesha shughuli zake Zamahero, Dodoma.
Kampuni hiyo ambayo inamilikiwa na Simon Mkondya ambaye ni maarufu kwa jina la Mr. Manguruwe, hivi sasa kwa miezi kadhaa, imeshindwa kuwalipa wawekezaji fedha ambazo walikubaliana kwa mujibu wa mikataba yao ambayo Afrika Leo imeiona.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo kupitia ‘Kijiji cha Nguruwe Project’,’ mwekezaji atalipwa sehemu ya faida itakayopatikana kila siku, wiki au mwezi kulingana na muhusika atakavyoamua na atalipwa kulingana na kiwango alichowekeza.
“Mimi nina miezi mitatu sasa nasotea hela yangu, tangu nilipowekeza nimepokea faida mara moja tu kwenye akaunti yangu, baada ya hapo sijaona chochote, nikaamua kwenda kwenye ofisi zao maeneo ya Sinza, hakuna nilichoambulia zaidi ya ahadi ambazo hazitekelezeki na kibaya zaidi wasimamizi wa hiyo ofisi niliowakuta wanatoa lugha kali za kukatisha tamaa,” alisema mmoja wa wawekezaji ambaye hakupenda jina lake liwekwe wazi kwasasa.
Alisema, mara zote alizokwenda kwenye ofisi za kampuni hiyo, alikuta idadi kubwa ya watu wanaodai na wengine hawajalipwa kwa miezi mingi zaidi, na wapo ambao wamewekeza kiasi kikubwa cha fedha zaidi yake ambaye aliweka Shilingi 2,000,000.
“Nimeshangaa kukuta mtu amewekeza fedha nyingi na hajalipwa chochote, halafu kuna wengine wanaendelea kujaza fomu kujiunga na mradi huu ambao niseme wazi una utapeli mwingi,” alisema na kuongeza kuwa, yeye ni mjane ambaye aliamua kuwekeza fedha zake ili faida imsaidie kumudu kuendesha familia yake, lakini ndoto zake zimepotea.
Alisema, ni miezi mitatu sasa anafuatilia fedha zake lakini hakuna mafanikio, huku wahusika akiwemo Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Simon Mkondya akiwakwepa na mara zote walipompigia hapokei simu, na hilo lipo kwa wasaidizi wake.
“Mkondya hapokei simu na hata wasaidizi wake ukija ofisini wanakupiga kalenda wanasema watakupigia ila ukiondoka ndio umeliwa, hawapigi, ukiwapigia hawapokei ni hadi uende ofisini kwao, kwa kweli ni jambo ambalo linachosha sana, tunaiomba Serikali itusaidie, maana tuliowekeza ni wengi sana na bado wanaendelea kuhamasisha watu wengine wawekeze,” alisema.
Taarifa zaidi zinadai kwamba, Mkondya kabla ya kuanzisha mradi huo alianzisha mradi wa Vannila, Mkoani Arusha ambako nako wengi walipoteza fedha zao, na kati ya wanaoendelea kudai wapo wawekezaji wa zao hilo ambao wanahangaika bila mafanikio.
“Kwanini nchi hii yetu imeanza kuchezewa na watu kiasi hiki na Serikali ipo kabisa inaangalia ni nini kinafanyika kwa mtu huyu anayeonekana kwenye matukio akitaka kutrend kwamba ana pesa wakati kaziliza familia kwa miradi FAKE,” alihoji mmoja watu ambaye ndugu zake wamepoteza fedha zao kupitia kampuni hiyo.
Aliendelea: “Jamaa amekuwa akiwapa mikataba FAKE watanzania na kuwaliza kwa miradi FAKE hivi hatujifunzi kuwa huyu jamaa ndio yule wa Vanilla sasahivi kawa Bwana Manguruwe ni hatua gani zinafuata baada ya hili kutokea?”
Aidha, kwa mujibu wa wawekezaji waliofanikiwa kufika kwenye shamba ambalo linaendeshwa mradi huo, idadi ndogo ya nguruwe waliowakuta imewakatisha tamaa, kwani ni dhahiri kwamba haiendani na idadi kubwa ya watu waliowekeza na mabanda mengi ni matupu.
Inadaiwa, nguruwe hao hawafiki 70 jambo ambalo linaonyesha wazi kiasi cha fedha kilichowekezwa hakiendani na uwekezaji ulifanyika, huku kukiwa na taarifa nyingine kwamba Mkondya amewaahidi wawekezaji kwamba anatafuta mkopo kwenye moja ya benki za hapa nchini ili kuwalipa fedha zao.
Hivi karibuni kupitia vyombo vya habari, Serikali kupitia kwa John Chasama ambaye ni Kaimu Msajili wa Bodi ya nyama alitembelea eneo la mradi huo na alisema, bodi hiyo imemsajili Mr. Manguruwe kama mfugaji mdogo na kwa mujibu wa kanuni za ufugaji, alitakiwa kuwa na mifugo isiyozidi 49.
Alisema, Mr. Manguruwe amekuwa akitoa taarifa kwa watanzania kwamba wawekeze kwenye mradi huo jambo ambalo sio sahihi na anavunja sheria kwa kuendelea kuita watu wawekeze wakati anajua idadi anayotakiwa kuwa nayo ni ndogo.
Mbali na hilo, alisema Mr. Manguruwe amekuwa akitoa taarifa nyingi za kupotosha kuhusu aina ya nguruwe anaowafuga, “amekuwa akisema ana nguruwe wa kipekee, wana uzito unaofikia Kilo 1400 na kuhusisha ulaji wa nguruwe hao na mabadiliko ya ukuaji wa maumbile ya akinamama.”
Alisema, kwa mujibu wa taarifa za sayansi za mifugo, taarifa anazotoa sio sahihi, hazina ukweli na anapotosha jamii “jambo hili sio sawa na aache mara moja,” alisisitiza Chasama na kuongeza, upotoshaji huo unaweza kuathiri soko la nyama kutoka nchini ikizingatiwa hivi sasa nchi ipo kwenye nafasi nzuri kwenye tasnia hiyo.
Chasama aliwataka wadau wote waliosajiliwa na bodi ya nyama kufuata sheria huku akiwasihi watanzania kuwa makini wanaposikia uwekezaji wa aina hiyo, ni vizuri wakatafuta taarifa za kutosha kwenye mamlaka zinazohusika ili kupata ukweli kabla ya kutoa fedha zao.
“Wawe makini, mamlaka zinazosimamia tasnia hii zipo, unapona jambo fika kwenye mamlaka husika upate ufafanuzi kuhusu taarifa ambazo zinakwenda kwenye mitandao ya kijamii,” alisema Chasama.
Hata hivyo, Simon Mkondya alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi hakupokea na hata alivyotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (SMS) licha ya kupokelewa, lakini hakuna majibu yoyote aliyoyatoa.